Simba SC |
Na Mahmoud Zubeiry
MABINGWA watetezi, Simba SC leo wanashuka dimbani kwenye
Uwanja wa Mkwakwani, Tanga kumenyana na wenyeji Mgambo JKT katika mfululizo wa
Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Simba SC wako mjini Tanga tangu juzi jioni kwa ajili ya mechi
yao ya leo inayotarajiwa kuwa kali nay a kusisimua, kulingana na hali
ilivyobadilika ghafla katika Ligi Kuu hivi sasa.
Simba iliyoanza Ligi Kuu kwa kishindo, ikishinda mechi sita
mfululizo, imelazimishwa sare katika mbili mfululizo zilizopita 0-0 na Coastal
Union mjini Tanga na 2-2 na Kegara Sugar mjini Dar es Salaam na leo imepania
kumaliza mdudu wa sare.
Kocha Mserbia, Profesa Milovan Cirkovick amesema yeye na
wachezaji wake wamejifunza jambo baada ya sare ya pili na Kagera Jumatano na
sasa wataongeza juhudi zaidi ili kuhakikisha matokeo hayo hayajirudii.
Lakini Mgambo nayo, iliyoanza Ligi kizembe, imezinduka na
kushinda mechi tatu mfululizo, tena moja ya ugenini dhidi ya Mtibwa Sugar 2-1
wiki iliyopita kabla ya kushinda 2-0 dhidi ya Toto African mjini Tanga.
Simba ipo Tanga na wachezaji wake 24, ambao ni makipa; Juma
Kaseja Juma, Wilbert Mweta William na Waziri Hamad Mwinyiamani, mabeki Nassor
Said Masoud ‘Chollo’, Amir Maftah Mrisho, Paulo George Ngalema, Koman Bili
Keita, Pascal Ochieng Akullo, Hassan Hatibu Kondo.
Viungo ni Jonas Mkude Gerrald, Ramadhani Chombo Redondo, Amri
Kiemba Athumani, Abdallah Omar Seseme, Ramadhani Singano Yahya, Uhuru Selemani
Mwambungu, Mrisho Khalfan Ngassa, Mwinyi Kazimoto Mwetula na Salim Abdallah
Kinje na washambuliaji Abdallah Juma, Daniel Akuffo, Felix Mumba Sunzu, Edward
Christopher Shija, Haruna Athumani Chanongo na Emmanuel Arnold Okwi.
Waliobaki Dar es Salaam ni Haruna Moshi ‘Boban’
anayesumbuliwa na maumivu ya misuli, Haruna Shamte, anayeumwa goti, Kigi Makassy
anayeumwa goti pia, Shomari Kapombe anayesumbuliwa na maumivu ya kifundo cha
mguu na Juma Said Nyosso anayetumikia adhabu ya kadi (tatu za njano).
Simba bado inaongoza Ligi Kuu kwa pointi zake 18, baada ya
kucheza mechi nane, ikifuatiwa na Azam yenye pointi 17, baada ya kucheza mechi
saba, wakati Yanga iliyocheza mechi nane ni ya tatu kwa pointi zake 14.
Katika mchezo wa leo, huenda Milovan akawapanga mabeki Komal
Bil Keita kutoka Mali na Paschal Ochieng kutoka Kenya, kucheza pamoja kwa mara ya
kwanza tangu kuanza kwa Ligi Kuu, kwa sababu Juma Nyosso na Kapombe hawapo
wote.
Mechi nyingine za leo, JKT Ruvu itaonyeshana kazi na JKT
Oljoro kwenye Uwanja wa Chamazi, wakati Tanzania Prisons na Toto Africans
zitapimana ubavu kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.