Wachezaji wa Simba SC wakipasha |
Na Prince Akbar
SIMBA inaendelea vizuri kwa
maandalizi yake ya mchezo wa kesho dhidi ya wenyeji Coastal Union mjini Tanga
na wachezaji wote 22 waliokwenda huko wana morali ya kutosha ya ushindi.
Vigogo wa Friends Of Simba (F.O.S)
wakiongozwa na Mwenyekiti wao, Zacharia Hans Poppe wamekodi ndege kwenda Tanga
kuwaongezea morali washinde mechi ya kesho, ambayo inatarajiwa kuwa ngumu
kutokana wenyeji kupania kuwa timu ya kwanza kuifunga Simba msimu huu.
Ikumbukwe Simba imetoa sare moja ya
kufungana 1-1 na Yanga, Oktoba 3, mwaka huu katika mechi zake sita ilizocheza
sasa na nyingine zote tano imeshinda, jambo ambalo linawafanya waendelee kuwa
kileleni mwa Ligi Kuu.
Simba, ambayo kwenye mechi hiyo
itawakosa nyota wake saba, Emanuel Okwi ambaye amekwenda kujiunga na timu yake
ya taifa, Uganda, Ramadhani Chombo ‘Redondo’, Mrisho Khalfan Ngassa wanaosumbuliwa
na Malaria, Haruna Shamte, Kiggi Makassy Kiggi, Hamadi Waziri na Komabil Keita
ambao ni majeruhi ipo Tanga tangu juzi.
Wachezaji 22 walio na timu Tanga ni
makipa Juma Kaseja, Wilbert Mweta, mabeki Nassor Masoud ‘Chollo’, Amir Maftah, Juma
Nyoso, Paschal Ochieng, Shomary Kapombe, Hassan Khatib, Paulo Ngalema, Komabil
Keita, viungo Mwinyi Kazimoto, Jonas Mkude, Amri Kiemba, Salim Kinje, Ramadhani
Singano, Uhuru Suleiman, Haruna Moshi ‘Boban’ na washambuliaji Felix Sunzu,
Edward Christopher, Haroun Chanongo, Daniel Akuffo na Abdallah Juma.
Katika kujiandaa na mechi ya Tanga,
Simba Jumanne ilicheza mechi ya kujipima nguvu na kuifunga Azam FC mabao 3-2
katika mchezo wa kirafiki uliofanyika asubuhi kwenye Uwanja wa Chamazi, maarufu
kama Azam Complex, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Mabao ya Simba siku hiyo yalifungwa
Ramadhani Singano ‘Messi’, Uhuru Suleiman ‘Robinho’ na Daniel Akuffo, wakati ya
Azam yalifungwa na Jamil Mchauru na Khamis Mcha.
Hiyo ilikuwa mechi ya nne Azam
inafungwa na Simba msimu huu katika mechi tano walizokutana hadi sasa, baada ya
awali kufungwa kwa penalti kwenye fainali ya Kombe la Urafiki, kufuatia sare ya
2-2, kufungwa 2-1 kwenye Nusu Fainali ya BancABC Sup8R na 3-2 kwenye mechi ya
Ngao ya Jamii, wakati wao walishinda 3-1 dhidi ya Wekundu hao wa Msimbazi,
katika Robo Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame.
Azam na Simba zitakutana tena
katika mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, mzunguko wa kwanza, Oktoba
27, mwaka huu, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Simba ndio inaongoza Ligi Kuu, hadi
sasa ikiwa imeshinda mechi tano kati ya sita ilizocheza na moja tu imetoka
sare, hivyo kujikusanyia pointi 16, wakati Azam inashika nafasi ya pili
ikizidiwa pointi tatu, ingawa pia iko nyuma kwa mchezo mmoja.