Wachezaji wa Simba SC |
Na Mahmoud Zubeiry
SIMBA SC tangu jana wameendelea na mazoezi kujiandaa na
mchezo wao ujao dhidi ya Polisi mjini Morogoro katika mfululizo wa Ligi Kuu ya
Vodacom Tanzania Bara, wakitoka kushinda mabao 3-1 dhidi ya Azam FC Jumamosi na
kujiimarisha kileleni.
Mabingwa hao watetezi jana walifanya mazoezi kwenye Uwanja wa
Kinesi, Urafiki, Manzese, Dar es Salaam na kwa ujumla timu vizuri kuelekea
mchezo huo wa tatu kucheza nje ya Uwanja wa Taifa, msimu huu baada ya awali
kucheza mechi mbili Tanga dhidi ya Coastal Union na Mgambo JKT ambazo zote
walilazimishwa sare ya bila kufungana.
Simba imeshinda mechi zake zote Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam na kutoa sare mbili tu, dhidi ya mahasimu wao wa jadi, Yanga 1-1 na 2-2
dhidi ya Kagera Sugar ya Bukoba.
Wekundu hao wa Msimbazi, wapo kileleni mwa Ligi Kuu kwa pointi
zao 22 baada ya kucheza mechi 10, wakifuatiwa na wapinzani wao wa tangu enzi za
bibi na babu, Yanga SC wenye pointi 20 katika nafasi ya pili.
Beki Juma Said Nyosso na kiungo Haruna Moshi Shaaban ‘Boban’
wanaendelea kutumikia adhabu zao za kusimamishwa, lakini wachezaji wote wengine
wapo fiti kabisa, ukiondoa Obadia Mungusa aliyefukuzwa mapema tu kabla ya
kuanza kwa Ligi Kuu.
Simba inatarajiwa kuondoka kesho Dar es Salaam kwenda
Morogoro kwa ajili ya mchezo dhidi ya Polisi ambayo inashika mkia katika ligi
hiyo, ikiwa haijashinda hata mechi moja tangu kuanza kwa ligi hiyo zaidi ya
kutoa sare mbili.
Lakini hiyo haiifanyia Simba idharau mechi hiyo na kocha Mserbia,
Milovan Cirkovick ameanza maandalizi ya mapema kwa ajili ya mechi hiyo.
Hofu kubwa kwa Simba ni hali ya Uwanja wa Jamhuri, Morogoro-
ni mbaya na kulingana na uzoefu walioupata wa kucheza kwenye Uwanja mwingine mbovu
wa Mkwakwani, Tanga wanajua watakuwa na shughuli pevu keshokutwa.
Hadi sasa Simba ndio timu pekee katika Ligi Kuu, ambayo
haijapoteza mechi, ikiwa imeshinda mechi sita na kutoa sare nne.