Benjamin Effe wa Kagera Sugar akimdhibiti Mrisho Ngassa wa Simba katika mechi ya jana |
Na Princess Asia
MECHI ya Ligi Kuu ya Vodacom kati ya Simba na Kagera Sugar iliyochezwa
jana kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kumalizika kwa sare ya mabao 2-2
limeingiza sh. 58,505,000.
Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura
ameiambia BIN ZUBEIRY leo kwamba, watazamaji 9,842 walikata tiketi kushuhudia
mechi hiyo iliyochezwa kwa viingilio vya sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000, na
sh. 20,000 huku kila klabu ikipata mgawo wa sh. 11,013,785.54 wakati Kodi ya
Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 8,924,491.53.
Amesema mgawo mwingine wa mapato hayo ni posho ya msimamizi
wa kituo sh. 120,000, kamishna wa mechi sh. 250,000, waamuzi sh. 440,000,
mtathimini wa waamuzi sh. 254,000, mwamuzi wa akiba sh. 70,000, usafi na ulinzi
wa uwanja sh. 2,350,000 na Wachina (stadium technical support) sh. 2,000,000.
Amesema umeme sh. 300,000, maandalizi ya uwanja (pitch
preparation) sh. 400,000, ulinzi wa mechi sh. 3,500,000 wakati tiketi ni sh.
3,183,890. Gharama za mchezo sh. 3,671,261.85, uwanja sh. 3,671,261.85, Kamati
ya Ligi sh. 3,671,261.85, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh.
2,202,757.11 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh.
1,468,504.74.
Katika mechi hiyo, Simba ililazimishwa sare ya kufungana
mabao 2-2 na Kagera kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, hiyo ikiwa sare ya
pili mfululizo kwa Wekundu hao wa Msimbazi, baada ya Jumamosi pia kulazimishwa
sare ya bila kufungana na Coastal Union mjini Tanga.
Kwa matokeo hayo, Simba imefikisha pointi 18 na kuendelea
kuongoza Ligi Kuu, kutokana na Azam FC kulazimishwa sare ya bila kufungana na
Prisons kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.
Hadi mapumziko, Simba SC walikuwa mbele kwa bao 1-0,
lililotiwa kimiani na mshambuliaji wa kimataifa wa Zambia, Felix Mumba Sunzu
Jr. dakika ya nane, akiunganisha kwa kichwa krosi ya Nassor Masoud ‘Chollo’
kutoka wingi ya kulia.
Kwa ujumla kipindi cha kwanza timu zote zilishambuliana kwa
zamu, ingawa ni Simba walioonekana kufanya mashambulizi ‘yenye akili’ zaidi.
Kipindi cha pili Simba ilirudi na moto tena na katika dakika
ya 51, Mrisho Khalfan Ngassa aliifungia timu hiyo bao la pili kwa shuti kali
lililowababatiza mabeki wa timu hiyo na kutinga nyavuni.
Hilo lilikuwa bao la tatu kwa Ngassa tangu ajiunge na Simba
katika mechi tisa alizoichezea timu hiyo ya Mtaa wa Msimbazi.
Baada ya hapo, Kagera walizinduka na kuanza kulishambulia
lango la Simba kupitia pembeni na katika dakika ya 64 Themi Felix aliunganisha
kwa kichwa krosi ya George Kavilla na kuifungia Kagera bao la kwanza.
Bao liliwazindua Kagera, ambao waliongeza kasi ya
kulishambulia lango la Simba na katika dakika ya 66, Juma Nyosso alimkwatua
kwenye eneo la hatari Paul Ngwai na Salum Kanoni akaenda kumtungua Juma Kaseja,
akiisawazishia Kagera.
Baada ya hapo timu zilianza kushambuliana kwa zamu na mpira
ulinoga zaidi kutokana na mashambulizi ya pande zote mbili.