Wachezaji wa Simba kwa raha zao |
Na Mahmoud Zubeiry
SIMBA SC imezinduka kutoka kwenye wimbi la sare katika Ligi
Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, baada ya kufanikiwa kuichapa Azam FC mabao 3-1
kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Ushindi huo, unaifanya Simba izidi kujitanua kileleni mwa
ligi hiyo kwa kufikisha pointi 22, baada ya kucheza mechi 10, wakati Azam FC
inapromoka hadi nafasi ya tatu kwa pointi zake 18, baada ya kucheza mechi tisa,
ikiipisha Yanga nafasi ya pili, ambayo imetimiza pointi 20 baada ya kuifunga
JKT Oljoro leo.
Mabao ya Simba leo yalitiwa kimiani na Emanuel Arnold Okwi
mawili na Felix Mumba Sunzu Jr. moja, wakati la Azam lilifungwa na John Raphael
Bocco ‘Adebayor’.
Hadi mapumziko, tayari Simba walikuwa mbele kwa mabao 2-1,
Azam wakitangulia kufunga dakika ya nne, kupitia kwa Adebayor ambaye alimtoka
beki Mkenya Paschal Ochieng na kumchambua Juma Kaseja.
Dakika mbili baadaye, Sunzu aliisawazishia Simba,
akiunganisha kwa kichwa krosi maridadi ya Mrisho Khalfan Ngassa kutoka wingi ya
kulia.
Okwi aliifungia Simba bao la pili dakika ya 40, baada ya
kutokea kizaazaa langoni mwa Azam kufuatia mpira uliopigwa langoni mwa timu
hiyo na Mwinyi Kazimoto.
Kipindi cha pili Simba walirudi na moto wao na iliwachukua
dakika tano tu kuhitimisha karamu yao ya mabao, baada ya Okwi kuwainua tena
vitini mashabiki wa Simba, akifumua shuti la umbali wa mita 19, baada ya
kuwatoka mabeki wa Azam.
Mrisho Ngassa ndiye alikuwa nyota wa mchezo wa leo, kutokana
na kuisumbua mno Azam, iliyomuuza kwa mkopo Simba miezi miwili iliyopita.
Simba SC; Juma Kaseja, Nassor Masoud ‘Chollo’, Amir Maftah, Paschal
Ochieng, Shomary Kapombe, Jonas Mkude, Amri Kiemba/Ramadhan Chombo, Mwinyi
Kazimoto, Felix Sunzu/Ramadhan Singano, Mrisho Ngassa/Christopher Edward na Emmanuel
Okwi.
Azam FC; Mwadini Ali, Ibrahim Shikanda, Samir Hajji Nuhu,
Said Mourad na Aggrey Morris, Abdulhalim Humud, Jabir Aziz/Abdi Kassim, Himid
Mao/Kipre Balou, John Bocco ‘Adebayor’/Khamis Mcha, Kipre Herman na Salum
Abubakar.
Katika mchezo uliotangulia, Azam B iliifunga Simba B 1-0, bao
pekee la Kevin Friday dakika ya 56.
Kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha, Yanga
iliibuka na ushindi wa 1-0, bao pekee la beki Mbuyu Twite, hilo likiwa bao lake
la tatu tangu ajiunge na timu hiyo kwenye ligi hiyo.
Kwa ushindi huo, Yanga imetimiza pointi 20, baada ya kucheza
mechi 10 na kupanda nafasi ya pili.
Mechi nyingine za ligi hiyo leo ni kati ya African Lyon imetoka
sare ya 1-1 Kagera Sugar Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam, Ruvu Shooting imeifunga
2-1 Polisi Morogoro Uwanja wa Mabatini, Mlandizi.
Mechi kati ya Mgambo JKT na Prisons iliyokuwa ichezawe leo Uwanja
wa Mkwakwani, Tanga imeahirshwa kutokana na wachezaji wa Prisons kupata ajali
wakiwa njiani kuelekea Tanga.
Ligi hiyo itaendelea kesho kwa michezo miwili kati ya JKT
Ruvu na Coastal Union Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam na Toto Africans dhidi
ya Mtibwa Sugar Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.