Simba SC |
Na Mahmoud Zubeiry
LIGI Kuu ya soka ya Vodacom Tanzania Bara, leo inaingia katika
mzunguko wake wa nane kwa nyasi za viwanja vitano kuwaka moto, huku macho na
masikio ya wengi yakielekezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, ambako mabingwa
watetezi Simba watakuwa wenyeji wa Kagera Sugar kutoka Bukoba mkoani Kagera.
Mechi hiyo namba 52 itachezeshwa na refa Ronald Swai kutoka
Arusha, akisaidiwa na Julius Kasitu na Methusela Musebula, wote kutoka
Shinyanga na refa wa akiba atakuwa Ephrony Ndisa wa Dar es Salaam.
Kagera Sugar inayofundishwa na kocha na mchezaji wa zamani wa
Simba SC, Abdallah Kibadeni mara nyingi imekuwa timu ambayo inaonyesha upinzani
mkali inapokutana na Simba SC, iwe Dar es Salaam au Bukoba na leo inatarajiwa
kuwa hivyo pia.
Katika mchezo wa leo, huenda Simba ikaendelea kumkosa kiungo
wake hodari, Mrisho
Khalfan Ngassa ambaye pamoja na kuanza mazoeozi juzi na timu yake Simba SC,
lakini amesema bado hayuko sawa sawa.
Akizungumza
na BIN
ZUBEIRY juzi, Ngassa ambaye aliugua Malaria baada ya mechi dhidi ya
Yanga, Oktoba 3, mwaka huu alisema kwamba bado anahisi hana nguvu.
“Nimeanza
mazoezi na timu, lakini hata hivyo bado hali yangu haiko sawa sawa kwa kweli,
najisikia mwili hauna nguvu, hii Malaria ilinipelekesha sana, ila najikongoza
hivyo hivyo,”alisema Ngassa.
Lakini kuna
uhakika kwa kiungo mwingine wa Simba SC aliyekuwa anaumwa Malaria pia,
Ramadhani Chombo ‘Redondo’ akacheza leo,
kwa kuwa yeye yuko fiti asilimia 100.
Mbali na
Redondo, katika mchezo huo, Simba inatarajiwa kuwapokea wachezaji wake wengine watatu
iliyowakosa kwenye mechi iliyopita dhidi ya Coastal Union Jumamosi Uwanja wa
Mkwakwani, Tanga ambayo iliisha kwa sare ya bila kufungana, Emmanuel Okwi
aliyekuwa kwao Uganda kuichezea timu yake ya taifa, Komabil Keita, Haruna
Shamte na Kiggi Makasy waliokuwa majeruhi.
Mechi
nyingine za leo Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya utakuwa mwenyeji
wa mechi kati ya Tanzania Prisons inayofundishwa na Jumanne Chale na Azam iliyo
chini ya kocha Boris Bunjak kutoka Serbia. Nayo Polisi Morogoro iliyopanda
msimu huu itakuwa mwenyeji wa JKT Ruvu kwenye Uwanja wa Jamhuri.
Mgambo Shooting ambayo imepata ushindi mara mbili mfululizo
itakuwa nyumbani Uwanja wa Mkwakwani, jijini Tanga ikiikaribisha Toto Africans
katika mechi itakayochezeshwa na Geofrey Tumaini wa Dar es Salaam. Oljoro JKT
inayonolewa na Mbwana Makata itakuwa nyumbani Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh
Kaluta Amri Abeid jijini Arusha dhidi ya African Lyon.
Simba bado
ipo kileleni mwa Ligi Kuu kwa pointi zake 17, baada ya kucheza mechi saba,
ikifuatiwa na Azam FC yenye pointi 16, ambayo hata hivyo imecheza mechi sita,
wakati Yanga inashika nafasi ya tatu kwa pointi zake 11, baada ya kucheza mechi
saba pia.
REKODI YA SIMBA NA KAGERA:
Machi 3, 2012
Simba 3-1
Kagera Sugar
Septemba 18, 2011
Kagera Sugar
1-1 Simba
Machi 29, 2011
Simba 0-0
Kagera Sugar
Oktoba 27, 2010
Kagera Sugar
0-2 Simba
Februari 3, 2010
Kagera Sugar
1-1 Simba
Septemba 10, 2009
Simba 2-0
Kagera Sugar
Aprili 5, 2009
Kagera Sugar
0-2 Simba
Oktoba 14, 2008
Simba 1-0
Kagera Sugar
Aprili 19, 2008
Kagera Sugar
0-1 Simba
Oktoba 13, 2007
Simba 2-1
Kagera Sugar
Oktoba 18, 2006
Simba 2-1
Kagera Sugar
Juni 3, 2006
Kagera Sugar
1-0 Simba
(Kagera wakapewa
ushindi wa mezani
2-0, kwa Simba
kumchezesha Mussa
Mgosi akiwa ana kadi
tatu za njano)
Septemba 28, 2005
Kagera Sugar
0-2 Simba
Mei 25, 2005
Simba 0-1
Kagera Sugar