Samatta ataibeba Mazembe leo? |
Na Prince Akbar
TOUT Puissant Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
(DRC) leo ina mtihani mgumu mbele ya Esperance ya Tunisia katika mchezo wa
marudiano wa Nusu Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika mjini Tunis.
Hiyo inatokana na Mazembe kulazimishwa sare ya bila kufungana
na mabingwa hao wa Afrika, katika mchezo wa kwanza kwenye Uwanja wa Stade du TP
Mazembe mjini Lubumbashi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) wiki mbili
zilizopita.
Sare yoyote ya mabao inaweza kuivusha Mazembe hadi fainali,
lakini Esperance inapewa nafasi kubwa ya kushinda kwa kuwa itakuwa ikicheza
nyumbani.
Mchezo huo tayari umekuwa gumzo kubwa, kutokana na upinzani mkubwa
baina ya timu hiyo na hasa baada ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF),
kubadilisha refa wa mechi hiyo siku tatu kabla ya timu hizo kurudiana.
CAF imeteua marefa wapya wa kuchezesha mechi hiyo ya leo kufuatia
malalamiko yaliyowasilishwa na Mazembe dhidi ya refa Bakary Gassama kutoka
Gambia na sasa Badara Diatta wa Senegal ndiye ambaye sasa atachezesha mechi
hiyo mjini Tunis.
Magazeti nchini Tunisia yamepinga uteuzi wa refa mpya kwa
sababu anatoka nchi moja na kocha wa Mazembe, Lamine N’Diaye, ambaye ni
Msenegal pia.
Mazembe ina washambuliaji hatari wa Kitanzania, Mbwana Ally
Samatta na Thomas Emmanuel Ulimwengu ambao wote kwa sasa ni tegemeo la timu
hiyo.
Katika mchezo wa leo, Mazembe itamkosa beki wake tegemeo, Stopila
Sunzu aliyepewa kadi ya pili ya njano (nyekundu) dakika ya pili ya muda wa
nyongeza baada ya kutimu dakika 90 za kawaida kwenye mechi ya kwanza.
Awali, Sunzu kaka wa mshambuliaji wa Simba, Felix Sunzu,
alionyeshwa kadi ya kwanza ya njano dakika ya kwanza ya muda wa nyongeza baada
ya kutimu dakika 45 za kipindi cha kwanza.
Washambuliaji wote wawili wa Kitanzania walicheza mechi hiyo,
Mbwana Ally Samatta alicheza hadi dakika 83 alipompisha Sinkala, wakati Thomas
Emanuel Ulimwengu alitokea benchi dakika ya 58 kwenda kuchukua nafasi ya D.
Kanda.
Nusu Fainali nyingine ya michuano hiyo inatarajiwa kuchezwa
kesho kati ya mabingwa mara sita Afrika, Al Ahly ya Misri na Sunshine Stars ya
Nigeria mjini Cairo. Katika mechi ya kwanza ya iliyopigwa huko Ijebu-Ode kwenye
Uwanja wa kimataifa wa Dipo Dina, timu hizo zilitoka sare ya kufungana mabao
3-3.
Nahodha wa Sunshine, Godfrey Oboabona aliikosa mechi hiyo
baada ya kuonyeshwa kadi ya pili ya njano katika mechi ya mwisho ya makundi
dhidi ya Esperance ya Tunisia, wakati Mohamed Aboutrika alikuwa anatumikia
adhabu ya kufungiwa miezi miwili na Ahly.
Ahly ilipata bao la kwanza dakika ya 18 kupitia kwa Mohamed
Nagy, aliyefumua shuti kutoka nje ya boksi na kumtungua Moses Ocheje, kabla ya
Mahdy El Sayed kuifungia bao la pili timu hiyo dakika ya 30, wakati Sunshine
ilipata bao la kwanza dakika ya 40, kupitia kwa kiungo Mcameroon, Tamen Medrano
aliyemtungua kwa shuti la mbali kipa wa Ahly, Sherif Elkramy.
Wenyeji walisawazisha dakika ya 73 kwa mkwaju wa penalti wa
Dele Olorundare baada ya Ajani Ibrahim kuangushwa kwenye eneo la hatari na
Mohamed Nagy.
Pamoja na hayo, Mashetani Wekundu wa Cairo walipata bao
lililoelekea kuwa la ushindi, dakika moja badaaye kupitia kwa kijana mwenye
umri wa miaka 25, Nagy ambalo lilikuwa bao lake la pili kwenye mechi hiyo.
Beki wa Sunshine, Precious Osasco aliisawazishia timu yake
dakika ya 83 kwa shuti la mpira wa adhabu lililomshinda kipa Elkramy. Nagy alipata nafasi ya kukamilisha hat-trick
dakika tatu kabla ya filimbi ya mwisho, lakini kichwa chake kiliupaisha mpira
alipokuwa anaunganisha kona.