![]() |
Mathew Akrama |
Na Prince Akbar
KAMA ilivyotarajiwa
na wengi, refa Mathew Akrama wa Mwanza aliyechezesha ovyo mechi ya watani wa
jadi katika soka ya Tanzania, Simba na Yanga, Jumatano wiki hii Uwanja wa Taifa,
Dar es Salaam ‘amekwenda na maji’.
Taarifa ya
Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura imesema
kwamba, Kamati ya Ligi imewaondoa marefa watatu wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania
Bara, kutokana na kuvurunda.
Mbali na
Akrama ambaye ‘Yanga hawana hamu naye’ tangu siku hiyo, wengine ni Paul Soleji
wa Mwanza aliyechezesha mechi kati ya Simba na Tanzania Prisons, na mwamuzi
msaidizi namba mbili kwenye mechi hiyo Mwarabu Mumbi wa Morogoro, wakati mwamuzi
msaidizi namba mbili wa mechi ya Yanga na Simba, Ephrony Ndissa wa Dar es
Salaam amepewa onyo.
Kamishna wa
mechi namba 28 kati ya Yanga na African Lyon, Pius Mashera ameondolewa kwenye
orodha ya makamishna wa ligi hiyo kwa kuchelewa kufika kwenye kikao cha
maandalizi ya mechi (Pre match meeting) na uwanjani.
Vilevile
Mashera kwenye ripoti yake aliwasilisha malalamiko dhidi ya msimamizi wa kituo
cha Dar es Salaam, na kwa vile suala hilo ni la kinidhamu ametakiwa alipeleke
kwenye Kamati ya Nidhamu na Usuluhishi ya TFF.
Nayo Simba
imepigwa faini ya jumla ya sh. 600,000 kwa kuchelewa kufika kwenye pre match
meeting ya mchezo wao dhidi Tanzania Prisons (sh. 100,000) na kwa washabiki
wake kuwatupia chupa za maji waamuzi wa mechi hiyo (500,000).
Pia Kamati
ya Ligi imeagiza kuwa kwa vile suala la kipa Shaabani Kado wa Mtibwa Sugar
kudaiwa kumpiga kiongozi mmoja wa Ruvu Shooting mara baada ya mechi kati ya
timu hizo iliyochezwa Uwanja wa Azam Complex ni la kinidhamu lipelekwe kwenye
Kamati ya Nidhamu na Usuluhishi ya TFF.
0 comments:
Post a Comment