Rage |
Na Princess Asia
MWENYEKITI wa Simba SC, Alhaj Ismail Aden Rage amewataka wanachama
na wapenzi wa klabu hiyo kuwa watulivu na wasikatishwe na tamaa na sare tatu
mfululizo za timu hiyo katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, kwani safari
bado ni ndefu.
Rage amesema kwamba, hadi sasa timu yao haijafungwa katika
Ligi Kuu kuashiria kwamba bado ni timu bora na matokeo ya sare hizo tatu
mfululizo pia ni kutokana na uimara wa timu yao.
Rage ameonya wanachama wenye desturi ya kutoa maneno ya
uchochezi timu inapoyumba kidogo, waache kufanya hivyo kwa sababu wanaweza
kuvuruga amani iliyopo sasa klabuni.
Kikosi cha Simba kilirejea Dar es Salaam jana mchana kutoka
Tanga na kuingia kambini moja kwa moja kuanza maandalizi ya mechi ijayo ya Ligi
Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, dhidi ya Azam FC, Oktoba 27, mwaka huu, Uwanja wa
Taifa, Dar es Salaam.
Simba SC itakuwa na wiki nzima ya kujiandaa na mechi hiyo,
ikitoka kulazimishwa sare ya tatu mfululizo jana kwenye Uwanja wa Mkwakwani
mjini Tanga, baada ya kutoka 0-0 na wenyeji Mgambo Shooting katika mfululizo wa
Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Matokeo hayo, yanaifanya Simba ifikishe pointi 19, baada ya
kucheza mechi tisa na kuendelea kuongoza Ligi Kuu, ingawa wameuweka rehani
usukani wa ligi hiyo kwa Azam ambayo kesho inacheza na Ruvu Shooting Uwanja wa
Chamazi, Dar es Salaam.
Awali ya hapo, Simba ilitoka 2-2 na Kagera Sugar Uwanja wa
Taifa na 0-0 na Coastal Union Uwanja wa Mkwakwani.
Azam yenye pointi 17, ikishinda itafikisha pointi 20 na
kupanda kileleni, tena ikiwa nyuma kwa mchezo mmoja, kwani hadi sasa imecheza
mechi saba. Yanga iliyocheza mechi nane, ina pointi 14 katika nafasi ya tatu
nayo itacheza na Polisi Morogoro keshokutwa.