Wachezaji wa Prisons |
Na Mashaka Mhando,Tanga
UONGOZI wa klabu ya Tanzania Prison, umeliomba Shirikisho la
Soka Tanzania (TFF), kuahirisha mechi yao dhidi ya Ruvu Shooting ya Pwani inayotakiwa
kufanyika Jumatano ya Oktoba 31, kwenye Uwanja wa Mabatini Mlandizi, Pwani.
Katibu Mkuu wa timu hiyo, Sadiq Jumbe alisema wanaishukuru
TFF kwa kuahirisha mchezo wao uliopita dhidi ya Mgambo JKT uliokuwa upigwe
kwenye Uwanja wa Mkwakwani jana (Oktoba 27), kufuatia ajali ambayo timu yake
ilipata jana.
Alisema sababu kubwa ya kutaka mchezo huo nao uahirishwe ni
kutokana na wachezaji wake tegemeo kutokuwa katika hali nzuri, baada ya ajali hiyo.
"Kwa kweli ajali tuliyoipata ni kubwa, kila mtu mawazo
yake hayapo, achilia mbali wachezaji walioumia, tunatakiwa tukae muda
kutafakari na kuwapa nafasi wachezi walioumia kupumzika na kocha wetu aandae
wachezaji watakaochukua namba za waliopata ajali, sasa tunaomba TFF wauahirishe
pia mchezo wetu unaofuata dhidi ya Ruvu Shooting," alisema Jumbe.
Wachezaji sita wa Prison waliopata ajali ya basi usiku wa
kuamkia Alhamisi iliyopita katika eneo la Hale wilayani Korogwe na kulazwa katika
hospitali ya Teule iliyopo wilayani Muheza mkoani Tanga na kisha kuhamishiwa
katika hospitali ya mkoa Bombo, wameruhusiwa na hali zao zinaendelea vizuri.
Ajali hiyo ilitokea katika eneo hilo baada ya basi dogo, aina
ya Coasta lililowabeba wachezaji na viongozi wa timu hiyo wapatao 21 kuacha
njia na kupinduka wakati likiwa njiani kwenda Jijini Tanga.
Hiyo ilifuatia dereva wa gari hilo kushindwa kuumudu usukani,
baada ya kumulikwa na mwanga mkali wa taa za lori ambalo lilikuwa mbele yake
huku kukiwa na lori lingine pembeni ya barabara limepaki.
Katibu huyo alisema wanamshukuru Mungu kwa kupata nafuuu kwa
wachezaji wake na hatimaye kuweza kuruhusiwa kutoka hospitalini ingawa bado
wanakabiliwa na majeraha waliyoyapata katika miili yao.
Jumbe ambaye naye aliumia sehemu ya kifuani katika ajali hiyo
aliwataja wachezaji walioumia na kukimbizwa hospitalini kabla ya kuruhusiwa ni
Issa Mwantika, Lugano Mwangama, Khalid
Fungabreki, Daudi Masungwe ambaye alikuwa amepoteza fahamu na Misango Magai.