1.
Kamati ya Ligi jana (Oktoba 29,2012) ilifanya
kikao pamoja na klabu zinazoshiriki Ligi Kuu ya Vodacom kujadili mambo kadhaa,
likiwemo tukio la Jumamosi iliyopita la kuzuia televisheni na radio kutangaza moja
kwa moja michezo ya Ligi Kuu pamoja na wapiga picha za televisheni kuchukua
picha kwa ajili ya kutumia kwenye habari. Kamati ilifanya mazungumzo na
mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo (TASWA), Juma Pinto
kuhusu msukosuko huo na kufikia muafaka katika masuala yafuatayo:
a-
kwamba uamuzi wa kuzuia vituo vya redio na
televisheni kutangaza moja kwa moja ulikuwa sahihi lakini una kasoro katika
utekelezaji kwa kuwa hayakuwepo mawasiliano rasmi kwa vyombo vya habari na pia
haukutoa muda wa kutosha kwa vyombo hivyo vya habari kufanya maandalizi kwa
kadri ya utashi wa klabu za Ligi Kuu.
b-
Kwamba Kamati ya Ligi haijakataza redio
kutangaza moja kwa moja michezo ya Ligi Kuu, bali vituo vya redio ambavyo
vinataka kutangaza moja kwa moja michezo ya Ligi Kuu vifanye hivyo bila ya
kuweka matangazo ya wadhamini na kama matangazo hayo ya moja kwa moja
yatadhaminiwa, basi vituo hivyo havina budi kuwasiliana kwa maandishi na
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa maelekezo zaidi.
c-
Kwamba vituo vya redio vitakavyotaka kutangaza
moja kwa moja michezo ya Ligi Kuu, ni lazima zitamke mashindano hayo kuwa ni
“Ligi Kuu ya Vodacom”.
d-
Kwamba vituo vya televisheni vitakavyotaka
kutangaza moja kwa michezo ya Ligi Kuu ya Vodacom, ni lazima viingie mkataba na
TFF ambao utaaridhiwa na klabu husika. Kwa sasa, kituo cha televisheni cha Star
TV hakitaruhusiwa kurusha matangazo ya moja kwa moja ya michezo hiyo hadi hapo
mkataba utakaposainiwa na tunatumaini mkataba huo utasainiwa kabla ya mechi za
kesho na hivyo kuwapa fursa wapenzi wa soka wa maeneo mbalimbali kuendelea
kushuhudia Ligi Kuu ya Vodacom.
e-
Kwamba vituo vya televisheni vitakavyotaka
kuchukua picha kwa ajili ya habari zinaruhusiwa kufanya hivyo. Endapo kituo
hicho kitaonyesha mchezo uliorekodiwa, hatua zitachukuliwa dhidi ya kituo
hicho.
f-
Kamati inaomba radhi kwa usumbufu uliosababishwa
na uamuzi huo, lakini inazidi kusisitiza kuwa uamuzi huo ulifanywa kwa lengo
zuri la kuendelea kutafuta vyanzo vya fedha vitakavyoziwezesha klabu kujimudu
kiuchumi na kuifanya Ligi Kuu ya Vodacom iendeshwe kwa ubora zaidi.
Kim Poulsen |
2.
Kocha mkuu wa timu ya taifa ya Tanzania, Kim
Poulsen amerejea Dar es salaam baada ya kufanya ziara kwenye visiwa vya Pemba
na Unguja ambako alishuhudia mechi sita za Ligi Kuu ya Grand Malta kuanzia
Oktoba 19, 2012 hadi Oktoba 26, 2012 visiwani Zanzibar. Poulsen alishuhudia
mechi baina ya Falcom na Bandari iliyoisha kwa Falcom kushinda kwa mabao 3-1 na
pia mechi baina ya Duma na Bandari ambayo iliisha kwa Bandari kuibuka na
ushindi wa mabao 2-0. Mechi hizo mbili zilifanyika kisiwani Pemba.
Poulsen pia alishuhudia mechi zilizofanyika
kwenye Uwanja wa Amaan kisiwani Unguja ambako Mtendeni iliibwaga Chipukizi kwa
mabao 2-1; Mundu na Jamhuri (0-1), KMKM na Zimani Moto (1-0); na Mafunzo dhidi
ya Chuoni iliyoisha kwa Mafunzo kulala kwa mabao 3-0.
Poulsen amefurahishwa na ziara hiyo na
kusema kuwa ni kitu kizuri kwake na kwa soka la Tanzania kwa ujumla. Poulsen
alisema kuwa amefurahishwa na mapokezi aliyopata visiwani Zanzibar na
kukishukuru Chama cha Mpira wa Miguu cha Zanzibar (ZFA) kwa ushirikiano mkubwa
alioupata wakati wote akiwa Zanzibar.
Hata hivyo, Poulsen alisema hawezi kueleza
kwa sasa kama ameona wachezaji anaoweza kuwaita kwenye kikosi cha Taifa Stars,
lakini akasema amevutiwa na viwango vya wachezaji wengi.
3.
TFF inapenda tena kuihimiza klabu ya Yanga
kumalizana na mchezaji wake wa zamani, John Njoroge Mwangi kabla ya Novemba 2,
2012 ili ijiepushe na adhabu kaili inayoweza kuchukuliwa na Shirikisho la
Kimataifa la Vyama vya Mpira wa Miguu (FIFA). Kwa mujibu wa barua ya FIFA,
iwapo Yanga haitakuwa imemlipa mchezaji huyo na kusiwepo na mawasiliano yoyote,
shauri hilo litawasilishwa kwenye Kamati ya Nidhamu ya FIFA itakayokutana Novemba
14, 2012 kutathmini hukumu iliyotolewa mapema Januari mwaka huu.
4.
Mchezo namba 10 wa Ligi Daraja la Kwanza (FDL)
baina ya Morani na Polisi Tabora uliokuwa uchezwe Kiteto mjini Tabora Oktoba
31, 2012, sasa utachezwa Novemba 01, 2012 baada ya treni ambayo Morani walikuwa
wakisafiria kutoka kupata matatizo njiani wakati wakitoka Kigoma ambako
walicheza na Kanembo.
5.
TFF inapenda kutoa ufafanuzi wa taarifa
zilizotolewa na baadhi ya vyombo vya habari leo, likiwemo gazeti la Habari Leo
na Daily News, vikimnukuu rais wa TFF, Leodegar Tenga akisema kuwa amewataka
watu wanaotaka kugombea uongozi wa shirikisho watangaze nia ili wapate
kujadiliwa. Waandishi walioandika habari hiyo hawakumnukuu vizuri Rais Tenga
wakati akizungumzia masuala ya uchaguzi na hivyo kupotosha maana nzima ambayo
Ndg. Tenga alitaka iwafikie wapenzi wa michezo na hasa mpira wa miguu. Rais
Tenga alivitaka vyombo vya habari vianzishe mjadala utakaowashirikisha wapenzi
wa mpira wa miguu ili waelezee wanatarajia nini katika miaka ijayo na hivyo
kuwafanya viongozi watakaochaguliwa kufanya kazi kwa utashi wa maoni hayo ya
wananchi. Tunaelewa kuwa Rais Tenga ni muumini wa kuheshimu katiba, sheria na
kanuni na hivyo hawezi kutoa kauli ambayo inakiuka mchakato wa uchaguzi wa TFF
kwa kuwataka wanaowania uongozi kutangaza nia sasa badala ya kusubiri muda wa
kikanuni ufike. Ikumbukwe katika kikao chake na wahariri aliwahi kuulizwa swali
kama hilo na akasema kuwa akijibu lolote atakuwa amekiuka kanuni za uchaguzi
kwa kuwa itamaanisha anaanza kampeniu kabla ya muda. Ni vizuri waliohusika
wakafanya masahihisho ili kuzuia habari zao kutafsiriwa tofauti na wadau wa
mpira wa miguu na hivyo kuweka uwezekano wa kuvuruga mchakato wa uchaguzi.
6.
TFF imebadilisha tarehe ya kuanza kuchukua fomu
kwa watu wanaotaka kugombea uongozi wa Chama cha Mpira wa Miguu cha Dar es
salaam (DRFA) kwa lengo la kuhakikisha kuwa mchakato wa uchaguzi unafanyika kwa
mujibu wa kanuni. Kamati ya Uchaguzi ya DRFA ilitangaza jana kuwa uchukuaji
fomu ungeanza leo, lakini DRFA iliandikiwa barua jana kuelezwa kuwa mchakato
huo sasa utaanza kesho na uchaguzi utafanyika Desemba 12, 2012.
Mchakato wa uchaguzi wa viongozi wa DRFA
utakuwa kama ifuatavyo:
30/10/2012 Kamati
ya Uchaguzi DRFA kutangaza uchaguzi na nafasi
Zinazogombewa kwa mujibu wa katiba ya DRFA
31/10/2012 Kuanza
kuchukua fomu za kugombea uongozi
04/11/2012 Mwisho
wa kurudisha fomu ifikapo saa 10:00 alasiri
05-09/11/2012 Kamati ya Uchaguzi DRFA kupitia
fomu za waombaji uongozi na
kutangaza matokeo na kubandika kwenye mbao majina ya waombaji uongozi.
10-14/11/2012 Kutoa fursa ya pingamizi dhidi ya
waombaji uongozi. Pingamizi
ziwasilishwe kwa katibu wa Kamati ya Uchaguzi DRFA na
wawekaji pingamizi wazingatie Ibara ya 11 (2) ya Kanuni
za
Uchaguzi za Wanachama wa TFF.
15-17/11/2012 Kujadili pingamizi, usaili na
kutangaza matokeo ya usaili na
kuwajulisha kwa maandishi.
18-20/11/2012 Kukataa rufaa dhidi ya maamuzi ya
Kamati ya Uchaguzi ya DRFA
21-25/11/2012 Rufaa kusikilizwa na Kamati ya
Uchaguzi ya TFF na kutangaza
matokeo ya rufaa (Kama hakuna rufaa, Kamati ya Uchaguzi
ya
DRFA kutangaza majina ya wagombea na nafasi wanazogombea
na kuanza kampeni).
26/11/2012 Baada
ya maamuzi ya Kamati ya Uchaguzi ya TFF, Kamati ya
Uchaguzi ya DRFA kutangaza majina ya wagombea na nafasi
zao
na kuanza kwa kampeni
12/12/2012 Uchaguzi