Okwi |
Na Mahmoud Zubeiry
MABAO mawili aliyofunga mshambuliaji wa kimataifa wa Uganda, Emmanuel
Okwi jana katika mechi dhidi ya Azam FC Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam jana
yanamaanisha mambo mawili makubwa kwake.
Kwanza yamemsafisha mbele ya mashabiki wa timu hiyo, kufuatia
tuhuma za aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Kassim Mohamed Dewji kwamba
haitumikii kwa moyo safi klabu hiyo na pia yamepandisha thamani yake katika
kipindi hiki cha mazungumzo ya kusaini mkataba mpya.
Mzambia Felix Sunzu ndiye anayelipwa mshahara mkubwa zaidi
Simba SC, Sh. Milioni 5 na Okwi anayelipwa Sh. Milioni 2 anataka alipwe zaidi
kwa sababu anaamini ndiye anayeibeba zaidi timu hiyo.
Baada ya mechi ya jana, gumzo kubwa kwa mashabiki wa Simba
lilikuwa ni bao la pili alilofunga Okwi- kwamba lilikuwa zuri mno na wanaamini
hakubahatisha, kwa sababu amekuwa akifunga mabao kama hayo mara kadhaa.
Pamoja na hayo, katikati zilibuliwa tuhuma kwamba Okwi ana
mapenzi na Yanga na amekuwa akiihujumu timu hiyo- huku habari nyingine zikisema
anataka kwenda Azam.
Okwi hakuwahi kuibuka kujibu tuhuma hizo, lakini shughuli
yake ya jana ni sawa na majibu, kwani mabao hayo pamoja na kuidhuru Azam,
lakini yameifanya Simba ijichimbie kileleni na kuwaacha wapinzani wao, Yanga.
Okwi pia anawapelekea ujumbe viongozi wa Simba kwa mabao yake
ya jana, waache kusikiliza maneno ya mitaani na kukumbuka wajibu wao kama viongozi
kwa kujitofautisha na mashabiki.