Juma Nyosso |
Na Prince Akbar
SIMBA SC imekubali kuvunja mkataba na beki wake Juma Said
Nyosso kulingana na maombi yake, na imemtaka afike kwa Mwenyekiti wa Kamati ya
Usajili, Zacharia Hans Poppe kujadili suala hilo.
Habari za ndani kutoka Simba SC, zimesema kwamba Nyosso
amewasilisha maombi ya kuvunja mkataba na klabu hiyo, baada ya kushushwa kikosi
cha pili, akidaiwa kiwango chake kimeshuka hivyo amepewa fursa ya kwenda
kukiboresha.
Lakini Nyosso mwenyewe ameona kama hastahili kushushwa timu
ya pili na ameomba asitishiwe mkataba wake aondoke, jambo ambalo uongozi wa
klabu umelikubali.
Nyosso si kama anatuhumiwa kuhujumu timu, bali anaambiwa uwezo
wake umeshuka mno na kwamba amekuwa akiigharimu timu katika siku za karibuni,
hivyo amepewa fursa ya kwenda kupandisha kiwango chake.
Adhabu kama hii amewahi kupewa mshambuliaji wa kimataifa wa
Argentina, Carlos Tevez katika klabu ya Manchester City ya England msimu uliopita
na aliitumikia vizuri hadi aliporejeshwa tena kikosi cha kwanza, ambako
aliisaidia timu kumalizia msimu vizuri kwa kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu.
Mbali na Nyosso, kiungo Haruna Moshi Shaaban amesimamishwa kwa
wiki tatu kwa tuhuma za utovu wa nidhamu na katika kipindi hicho atakuwa
akipokea nusu mshahara.
Boban ameamua kurudi nyumbani kwake kupumzika na mkewe hadi adhabu
hiyo iishe ajue mustakabali wake, ila amesema anaonewa kwa sababu hakupewa
nafasi ya kujibu tuhuma zake kabla ya hatua kuchukuliwa, ingawa amechukulia poa
tu.
Wakati huo huo, habari zaidi kutoka ndani ya Simba, zimesema
kwamba Mwinyi Kazimoto Mwitula, Ramadhan Suleiman Chombo na Mrisho Khalfan
Ngassa nao wanaangaliwa kwa ‘jicho la tatu’ juu ya mwenendo wao kwenye timu
hiyo na kwa nyakati tofauti wote wamekwishaitwa kuhojiwa masuala mbalimbali.