Azam FC |
Na Mahmoud Zubeiry
LIGI Kuu ya soka ya Vodacom Tanzania Bara, inatarajiwa
kuendelea leo kwa nyasi za viwanja vitano kuwaka moto, huku macho na masikio ya
wengi yakiwa katika Viwanja vya Taifa, Dar es Salaam ambako Simba na Azam FC
zitakuwa zikimenyana na Sheikh Amri Abeid mjini Arusha, ambako Yanga SC watakuwa
wageni wa JKT Oljoro.
Lakini mechi kali zaidi itakuwa kati ya Azam na Simba ambazo
zitagombea usukani wa ligi hiyo, zikiendeleza upinzani wao wa tangu msimu uliopita
zilipogombea ubingwa.
Simba ndio inaongoza Ligi Kuu kwa pointi zake 19 wakati Azam
FC ina pointi 18 na Yanga yenye pointi 14, inashika nafasi ya tatu.
Dhahiri Azam ikishinda leo itapanda kileleni na hali itakuwa
mbaya zaidi kwa Simba iwapo na Yanga itashinda, kwani mabingwa hao watetezi
watakuwa wanawazidi wapinzani wao wa jadi kwa pointi mbili tu.
Azam ipo kambini kwake Chamazi, nje kidogo ya Jiji la Dar es
Salaam ilipokuwa ikijifua vikali chini ya kocha wake Mserbia, Boris Bunjak,
wakati Simba SC waliweka kambi visiwani Zanzibar tangu Jumanne kujiandaa na
mechi ya leo.
Simba iliyokuwa bingwa msimu uliopita na Azam iliyoshika
nafasi ya pili, ndizo timu pekee ambazo hadi sasa hazijafungwa hata mechi moja
katika Ligi Kuu.
Simba imetoa sare nne, dhidi ya Yanga (1-1), Coastal Union na
Mgambo (zote 0-0) na Kagera Sugar (2-2) wakati Azam imetoa sare tatu, 2-2 na
Toto Africans, 0-0 na Prisons na 1-1 na Ruvu Shoting.
Mechi ya leo itakuwa kipimo kingine cha kocha Mserbia wa
Azam, Bunjak ambaye hadi sasa amekwishaiongoza timu hiyo katika mechi 15 tangu
awasili nchini kurithi mikoba ya Muingereza, Stewart Hall, Agosti mwaka huu
kati ya hizo akiwa ameshinda tisa, sare tatu na kufungwa tatu.
Mechi zote alizofungwa ni dhidi ya Simba, 2-1 kwenye Nusu
Fainali ya BancABC Sup8R, 3-2 kwenye Ngao ya Jamii na 3-2 katika mchezo wa kirafiki
uliopigwa Chamazi.
Hivyo leo Bunjak atakuwa na wajibu wa kuwaridhisha matajiri wenye
asili ya Kiarabu, wanaoimiliki timu hiyo, kwamba yeye si mnyonge kwa Mserbia
mwenzake anayeinoa Simba SC, Profesa Milovan Cirkovick.
Simba baada ya sare ya tatu mfululizo ikaamua kwenda kuweka
kambi Zanzibar kujiandaa na mechi ya leo na kwa kawaida Wekundu wa Msimbazi
wamekuwa wakienda visiwani humo katikati ya Ligi kuweka kambi, wanapokuwa
wanajiandaa na mechi dhidi ya mahasimu wao tu, Yanga.
Kitendo cha kwenda Zanzibar kinamaanisha Simba wanaupa uzito
mkubwa mchezo huo wa leo- sawa tu na mchezo dhidi ya Yanga.
Lakini pia kambi ya Simba imekumbwa na mtikisiko kidogo
kuelekea mechi hii, kiasi cha kuwasimamisha wachezaji wake wawili beki Juma
Nyosso aliyeambiwa afanye mazoezi ni kikosi cha pili ili kuboresha kiwango
chake na kiungo Haruna Moshi ‘Boban’, ambaye amesimamishwa kwa wiki tatu kwa
utovu wa nidhamu.
Pamoja na hayo, bado kuna wachezaji ndani ya Simba
wanaangaliwa kwa jicho la tatu juu ya mwenendo wao, wakiwemo beki Amir Maftah,
viungo Ramadhan Chombo, Mwinyi Kazimoto na Mrisho Ngassa.
Safu ya ulinzi ya Simba itakuwa tena na beki wake chipukizi
mahiri, Shomary Kapombe ambaye amekosa mechi mbili zilizopita kutokana na
maumivu ya kifundo cha mguu na leo anaweza akacheza pamoja na Hassan Kondo
katika beki ya kati.
Hayatarajiwi mabadiliko makubwa sana kwenye kikosi cha Simba leo,
Juma Kaseja akiendelea kusimama langoni, kulia Nassor Masoud ‘Chollo’, kushoto
Amir Maftah, katikati Kapombe na Kondo, kiungo mkabaji Amri Kiemba, kulia
Mrisho Ngassa, katikati Mwinyi Kazimoto, kushoto Emmanuel Okwi na washambuliaji
Felix Sunzu anaweza akaanza na kinda Christopher Edward leo.
Azam bila shaka Mwadini Ali atasimama langoni, kulia Ibrahim
Shikanda, kushoto Erasto Nyoni, katikati Said Mourad na Aggrey Morris, kiungo
mkabaji Abdulhalim Humud, kulia Kipre Tcheche, kushoto Kipre Balou, katikati Salum
Abubakar na washambuliaji John Bocco ‘Adebayor’ na Abdi Kassim ‘Babbi’.
Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha, Yanga haitarajiwi
kuwa na mabadiliko makubwa sana katika kikosi chake kutoka kile kilichoshinda
3-0 dhidi ya Polisi katika mchezo uliopita.
Ally Mustafa ‘Barthez’ anaweza kuendelea kusimama langoni,
kulia Juma Abdul, kushoto Oscar Joshua, katikati Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na
Mbuyu Twite, kiungo mkabaji Athumani Iddi ‘Chuji’, kulia Simon Msuva, kushoto David
Luhende, katikati Haruna Niyonzima na washambuliaji Didier Kavumbangu na Jerry
Tegete.
JKT Oljoro; Shaibu Issa, Yussuf Nachogote, Nafo Zuberi au Jackson
Semfukwe, Salim Mbonde, Marcus Raphael (Nahodha), Emanuel Memba, Karage Gunda,
Saleh Iddi au Amir Omar, Paul Nonga, Meshack Nyambele na Sixbert Mohamed au Essau
Sanu.
Mechi nyingine za ligi hiyo leo ni kati ya African Lyon na
Kagera Sugar Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam, Mgambo JKT na Prisons Uwanja wa Mkwakwani,
Tanga na Ruvu Shooting dhidi ya Polisi Morogoro Uwanja wa Mabatini, Mlandizi.
Ligi hiyo itaendelea kesho kwa michezo miwili kati ya JKT
Ruvu na Coastal Union Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam na Toto Africans dhidi
ya Mtibwa Sugar Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
Simba SC |
REKODI YA SIMBA NA AZAM LIGI KUU:
Februari 11, 2012
Simba SC 2 - 0 Azam FC
Sept 11, 2011
Azam FC 0 - 0 Simba SC
Jan 23, 2011
Simba 2-3 Azam (Dar).
Sep 11, 2010
Azam 1-2 Simba (Tanga).
Machi 14, 2010
Azam 0-2 Simba (Dar)
Okt 24, 2009
Simba 1-0 Azam (Dar)
Machi 30, 2009
Azam 0-3 Simba (Dar)
Okt 4, 2008
Simba 0-2 Azam
Yanga SC |
YANGA NA OLJORO MSIMU ULIOPITA:
Aprili 25, 2012
JKT Oljoro 1 – 4 Yanga
Oktoba 23, 2011
Yanga 1 – 0 JKT Oljoro
JKT Oljoro |