Ngassa |
Na Prince Akbar
VIUNGO wa zamani wa Yanga, Mrisho
Khalfan Ngassa na Kiggi Makassy Kiggi wameenguliwa katika kikosi cha Simba
kilichoondoka leo kwenda Tanga kwa ajili ya mchezo wa Jumamosi wa Ligi Kuu ya
Vodacom Tanzania Bara, dhidi ya wenyeji Coastal Union kwenye Uwanja wa
Mkwakwani.
Ofisa Habari wa Simba SC, Ezekiel
Kamwaga amesema kwamba, Ngassa ameondolewa kwa sababu bado hajapona Malaria iliyomkosesha
mechi iliyopita ya ligi hiyo dhidi ya JKT Oljoro ya Arusha, wakati Makassy aliumia
jana kwenye mchezo wa kirafiki dhidi ya Azam FC.
Awali, Kamwaga alisema leo mchana kwamba,
katika safari hiyo timu hiyo itawakosa nyota watano, Emanuel Okwi ambaye
amekwenda kujiunga na timu yake ya taifa, Uganda, Ramadhani Chombo ‘Redondo’
anayesumbuliwa na Malaria, Haruna Shamte, Hamadi Waziri na Komabil Keita ambao
ni majeruhi.
Aliwataja wachezaji 22 waliokwenda na
timu Tanga ni makipa Juma Kaseja, Wilbert Mweta, mabeki Nassor Masoud ‘Chollo’,
Amir Maftah, Juma Nyoso, Paschal Ochieng, Shomary Kapombe, Hassan Khatib, Paulo
Ngalema, Komabil Keita, viungo Mwinyi Kazimoto, Jonas Mkude, Amri Kiemba, Salim
Kinje, Ramadhani Singano, Uhuru Suleiman, Haruna Moshi ‘Boban’ na washambuliaji
Felix Sunzu, Edward Christopher, Haroun Chanongo, Daniel Akuffo na Abdallah
Juma.
Katika kujiandaa na mechi ya Tanga,
Simba jana ilicheza mechi ya kujipima nguvu na kuifunga Azam FC mabao 3-2
katika mchezo wa kirafiki uliofanyika asubuhi kwenye Uwanja wa Chamazi, maarufu
kama Azam Complex, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Mabao ya Simba leo yalifungwa
Ramadhani Singano ‘Messi’, Uhuru Suleiman ‘Robinho’ na Daniel Akuffo, wakati ya
Azam yalifungwa na Jamil Mchauru na Khamis Mcha.
Hiyo ilikuwa mechi ya nne Azam
inafungwa na Simba msimu huu katika mechi tano walizokutana hadi sasa, baada ya
awali kufungwa kwa penalti kwenye fainali ya Kombe la Urafiki, kufuatia sare ya
2-2, kufungwa 2-1 kwenye Nusu Fainali ya BancABC Sup8R na 3-2 kwenye mechi ya
Ngao ya Jamii, wakati wao walishinda 3-1 dhidi ya Wekundu hao wa Msimbazi,
katika Robo Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame.
Azam na Simba zitakutana tena
katika mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, mzunguko wa kwanza, Oktoba
27, mwaka huu, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Simba ndio inaongoza Ligi Kuu, hadi
sasa ikiwa imeshinda mechi tano kati ya sita ilizocheza na moja tu imetoka
sare, hivyo kujikusanyia pointi 16, wakati Azam inashika nafasi ya pili
ikizidiwa pointi tatu, ingawa pia iko nyuma kwa mchezo mmoja.