Na Prince Akbar
SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko
taarifa za vifo vya wachezaji watano wa timu ya Rusumo FC ya mkoani Kagera
vilivyotokea jana jioni (Oktoba 16 mwaka huu).
Ofisa Habari wa TFF, Boniphace Wambura Mgoyo ameiambia BIN
ZUBEIRY leo kwamba Rusumo FC ilikuwa ikitoka kwenye mechi ya michuano
ya Polisi Jamii Wilaya ya Ngara ambapo ikiwa njiani kurudi Rusumo kutoka mjini
Ngara ilipata ajali ya gari na wachezaji watano kufariki papo hapo.
Alisema wachezaji wengine ambao ni majeruhi wamelazwa
Hospitali ya Wilaya ya Ngara ya Murugwanza huku wawili hali zao zikiwa mbaya.
Alisema msiba huo ni pigo kwa familia za marehemu, klabu ya
Rusumo FC, Chama cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Ngara (NDFA), Chama cha Mpira wa
Miguu Mkoa wa Kagera (KRFA) na familia ya mpira wa miguu kwa ujumla nchini
kutokana na mchango wa wachezaji hao katika ustawi wa mchezo huu kupitia klabu
yao.
“TFF inatoa pole kwa familia za marehemu, Rusumo FC, NDFA na
KRFA na kuwataka kuwa na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo
mzito. Kutokana na msiba huo, mechi zote za Ligi Kuu ya Vodacom zinazochezwa
leo (Oktoba 17 mwaka huu) kutakuwa na dakika moja ya maombolezo ili kutoa
heshima kwa marehemu hao. Mungu aziweke roho za marehemu mahali pema peponi,”alisema
Wambura.
Wakati huo huo: Wambura amesema kwamba Kocha Mkuu wa timu ya taifa,
Taifa Stars, Mdenmark Kim Poulsen wikiendi hii ataanza ziara ya Zanzibar
kuangalia Ligi Kuu ya Zanzibar.
Alisema Kim anatarajia kushuhudia mechi zilizopungua tano
akianzia kisiwani Pemba ambapo kati ya Oktoba 19 na 21 atashuhudiwa mechi mbili
zitakazochezwa kwenye Uwanja wa Gombani. Mechi hizo ni kati ya mabingwa
watetezi wa Ligi Kuu ya Grand Malta, Super Falcon ambao watacheza na vinara wa
ligi hiyo Bandari, na baadaye mechi kati ya Duma na Bandari.
“Baadaye atakwenda Unguja kwenye Uwanja wa Amaan
ambapo baadhi ya mechi alizopanga kushuhudia ni kati ya Mtende na Chipukizi,
Mundu na Jamhuri na KMKM dhidi ya Zimamoto,”alisema Wambura.