Amir Mhando |
Na Prince Akbar
CHAMA cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA), imefikia
hatua ya mwisho ya mazungumzo na mdhamini wa Mkutano Mkuu unaotarajiwa
kufanyika mwezi ujao katika tarehe ambayo itatangazwa rasmi.
Katibu Mkuu wa TASWA, Amir Mhando ameiambia BIN ZUBEIRY leo
kwamba, Kamati ya Utendaji ya TASWA ilikubaliana katika kikao chake mwezi
uliopita kuwa Mkutano Mkuu wa TASWA mwaka huu uwe wa aina yake kwa kuwawezesha
wanachama kukaa pamoja na kubadilishana mawazo na ikashauri ikiwezekana
ufanyike nje ya Dar es Salaam kama hali itaruhusu.
Amesema kutokana na hali hiyo, kikao kiliiagiza sekretarieti
ya TASWA itafute mdhamini wa kufanikisha suala hilo na kwamba kama
ikishindikana mkoani ifanyike Dar es Salaam lakini kuwe na mdhamini.
Amesema tayari hilo limefanyika na mdhamini amepatikana,
ambapo hatua ya mwisho ya mazungumzo na mdhamini itakuwa mapema wiki ijayo na baada ya hapo itatangazwa tarehe rasmi.
“Nichukue nafasi hii kuwaomba wanachama ambao hawajalipa ada
zao wafanye hivyo kwa kuwasiliana na Mhazini wa chama au Mhazini Msaidizi ili
waepuke usumbufu wa kushindwa kuhudhuria mkutano huo,”alisema Mhando.
Wakati huo huo: TASWA imempongeza mwanachama wake, Boniface
Wambura kwa kuteuliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu la Afrika (CAF) kuwa
mmoja wa maofisa watakaoshughulikia masuala ya habari wakati wa fainali za
Mataifa ya Afrika kwa Wanawake zitakazofanyika nchini Equatorial Guinea.
Mhando amesema TASWA imepokea kwa furaha uteuzi huo wa
Wambura ambaye ni Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na inaamini
ataendelea kufanya vizuri kama anavyotekeleza majukumu yake ya kazi ndani ya
TFF.
“Tangu Wambura aanze kazi ya Ofisa Habari wa TFF kumekuwa na
mapinduzi makubwa yanayohusiana na mambo ya habari na katika hili waandishi wa
habari za michezo nchini ni mashahidi wa hilo kwani amekuwa mtu sahihi kwao na
amekuwa na ushirikiano mkubwa usio na kifani kwa wanahabari wenzake,”alisema.
Mhando amesema kwa kuwa Wambura ni mwanachama hai wa TASWA,
kwa kuteuliwa kwake huko ni faraja kwa chama na tunamtakia kila la heri ili
aweze kutekeleza vyema majukumu yake kwani hiyo ni ishara tosha kwamba kazi
yake inaonekana na inathamanika.
Wambura ameteuliwa na Rais wa CAF, Issa Hayatou kwa ajili ya
kufanikisha uendeshaji wa fainali hizo za Mataifa ya Afrika kwa Wanawake
zilizopangwa kuanza Oktoba 28, 2012 na kumalizika Novemba 11, 2012, ambapo
atakuwa mmoja wa maofisa watatu watakaoshughulikia habari kwenye fainali hizo.
Wengine ni ofisa kutoka makao makuu ya CAF, Mahmoud Garga na Arlindo Macedo
kutoka Angola.