Daniel Akuffo mbele ya Mrisho Ngassa |
Na Mahmoud Zubeiry
KOCHA Mkuu wa
Simba SC, Profesa Milovan Cirkovick amesema kwamba mshambuliaji mpya kutoka Ghana,
Daniel Akuffo anatakiwa aongeze juhudi na kupandisha kiwango chake, ili apate
nafasi kwenye kikosi cha kwanza, lakini kwa sasa ataendelea kuanzia benchi kwa
kuwa anazidiwa uwezo na wachezaji wanaoanza.
Akizungumza baada
ya mechi dhidi ya JKT Oljoro juzi, Mserbia huyo alisema kwamba Akuffo anaanzia
benchi kwa sasa kwa sababu kuna wachezaji walio vizuri mno zaidi yake na ndio
wanapewa nafasi. “Ajitahidi, atakapokuwa vizuri atapata nafasi ya kuanza, ila
kwa sasa anazidiwa na wanaoanza,”alisema Milovan.
Daniel
Akuffo aliyesajiliwa msimu huu kutoka ASEC Mimosa ya Ivory Coast, aliingia kwa
kishindo Simba akifunga katika mechi
nne mfululizo, lakini baada ya hapo kasi yake imezimika na amefikisha jumla ya
mechi 10, akiwa amefunga mabao matano tu, katika ligi bao moja tu. Katika mabao
hayo matano aliyofunga jumla hadi sasa mshambuliaji huyo mrefu, mawili ni ya penalti.
Simba SC juzi
ilizidi kujiimarisha kileleni mwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kufuatia
ushindi wa mabao 4-1 ilioupata kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam dhidi ya
JKT Oljoro ya Arusha, ambayo ilimaliza pungufu ya wachezaji wawili baada ya
kipa wake Shaibu Issa na mshambuliaji Meshack Nyambele kutolewa kwa kadi
nyekundu kipindi cha pili.
Katika mechi
hiyo iliyochezeshwa na refa Amon Paul wa Mara, aliyesaidiwa na Anold Bugabo wa
Singida na Charles Simon wa Dodoma, hadi mapumziko Simba walikuwa tayari mbele
kwa mabao 2-1, mabao yake yote yakitiwa kimiani na kiungo Amri Ramadhan Kiemba
katika dakika za 16 na 44, wakati la Oljoro lilifungwa na Paul Nonga dakika ya
29.
Kiemba
alifunga bao la kwanza akiunganisha krosi pasi ya Christopher Edward, wakati
bao la pili lilitokana na krosi ya Nassor Masoud ‘Chollo’, yote kutokana na
mashambulizi ya upande wa kulia.
Ilikuwa
rahisi kwa Kiemba kufunga mabao yote akiwa kwenye eneo la hatari, kutokana na
mabeki wa Oljoro kumuwekea ulinzi zaidi Felix Sunzu.
Nonga naye
alifunga bao lake baada ya kupewa pasi ndefu na kumpiga chenga kipa na Nahodha
wa Simba, Juma Kaseja upande wa kulia mwa Uwanja na kuutumbukiza mpira nyavuni
kiulaini.
Bao hilo
lilitokana na beki Paul Ngalema kupokonywa mpira wakati amepanda kusaidia
mashambulizi na Oljoro wakafanya shambulizi la haraka.
Kipindi cha
pili Simba walirudi vizuri zaidi uwanjani na kuuteka zaidi mchezo- jambo ambalo
liliwafanya Oljoro wawapunguze kasi kwa kuwachezea rafu. Hilo liliwagharimu
kupoteza wachezaji wao wawili kabla ya filimbi ya mwisho na kufungwa mabao
mawili zaidi.
Dakika ya 83
Mganda Emanuel Okwi aliifungia Simba bao la tatu na katika dakika ya tatu ya
muda wa nyongeza baada ya kutimu dakika 90 za mchezo, Okwi akiwa anaelekea
kufunga tena, alikwatuliwa na kipa wa Oljoro Shaibu Issa na refa akaamuru
penalti sambamba na kumtoa nje kwa kadi nyekundu ya moja kwa moja mlinda mlango
huyo.
Awali ya
hapo, Oljoro ilimpoteza mchezaji mwingine, Nyambele dakika ya 78, ambaye
alionyeshwa njano ya pili kwa rafu aliyomchezea Jonas Mkude. Nahodha Kaseja
alitaka kwenda kupiga, lakini akazuiwa na Felix Mumba Sunzu akaenda kufunga bao
la nne kwa mkwaju wa penalti.
Kwa ushindi
huo, Simba imefikisha pointi 16 baada ya kucheza mechi sita, hivyo kuendelea
kuongoza Ligi Kuu, ikifuatiwa na Azam yenye pointi 13, ingawa imecheza mechi
tano.