Kikosi cha Mgambo JKT |
Na Mashaka Mhando, Tanga
TIMU ya soka ya Mgambo JKT ya mjini Handeni mkoani Tanga,
imeondoka leo mjini Tanga, ilikokuwa imeweka kambi kwenda Dar es salaam ambako
kesho itashuka dimbani kwenye Uwanja wa Taifa kucheza na wenyeji Yanga katika
mfululizo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Mgambo inayoshika nafasi ya 10 kwenye msimamo wa Ligi Kuu
hadi sasa kwa kuwa na pointi 10 ikiwa imecheza michezo tisa, imeondoka na wachezaji
wake 22 na viongozi watatu kwa ajili ya pambano hilo ambalo timu hiyo ilisema
kuwa inalichukulia kwa umakini mkubwa ili waweze kuibuka na ushindi kutokana na
kujiandaa vilivyo.
Kocha Mkuu wa timu hiyo Mohamed Kampira, alisema jana mjini
hapa kwamba, Yanga waailichukulie kuwa watawafunga kirahisi katika mchezo huo
badala yake wategemee kupata upinzani hasa kutokana na kwamba timu hiyo ya
Mgambo imejiandaa kuibuka na ushindi ili waweze kukaa katika nafasi nzuri
katika mzunguko huu wa kwanza.
"Tunaondoka kesho asubuhi (leo) kwenda Dar es salaam,
kama timu tumejiandaa vizuri na tunatarajia kuwapa wakati mgumu Yanga na
kuishinda, wasitarajie mteremko, sisi ni timu na tunaamini kwamba tutaibuka na
pointi zote tatu," alisema kwa kujiamini Kampira aliyevaa viatu vya
aliyekuwa kocha mkuu wa timu hiyo Stephen Matata aliyetimuliwa baada ya timu
hiyo kuanza vibaya kwa kufungwa michezo mitano mfululizo tangu kuanza kwa ligi
hiyo.
Kampira alisema hadi sasa wachezaji wake wamekuwa na ari
kubwa ya kuibuka na ushindi na hakuna majeruhi wote wapo katika hali nzuri ya
kupambana na timu hiyo inayousaka ubingwa mwaka huu kwa udi na uvumba na kwamba
amewata mashabiki wa timu hiyo kuiamini kwa wachezaji watafanya kazi
iliyokusudiwa.
Mgambo JKT ambayo baada ya kumtimua kocha ilikuwa imeshikwa
na kocha msaidizi Josepj Lazaro ambaye aliipa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya
Polisi Morogoro, akaifunga Mtibwa Sugar bao 2-1 kwenye uwanja wa Manungu,
ikaifunga Toto African bao 2-0 na ikatoka sare ya 0-0 na Simba mchezo ambao
Kampira ilikuwa ni mchezo wake wa kwanza kukaa kwenye benchi la timu hiyo.
Wakati huo huo, mashabiki wa klabu ya Coastal Union ya Jijini
hapa, wameipongeza timu yao kwa ushindi walioupata juzi walipoifunga JKT Ruvu
bao 3-0 katika mchezo uliofanyika kwenye uwanja wa Azam Complex, Chamazi Jijini
Dar es salaam hatau ambayo walisema inatia faraja na wamewataka wacheji wazidi
kuongeza bidii ili lengo la kumaliza ikiwa nafasi za juu litimie.
Mmoja wa mashabiki hao Fred Tayasar alisema wamejisikia
furaha ushindi huo lakini pia umewapa majonzi makubwa kwa mchezaji wao Nsa Job
kuvunjika mguu katika pambano hilo hatua ambayo alisema wapenzi wa timu hiyo
wanaangalia uwezekano wa kumchangia fedha kwa ajili ya kumpa ili aweze kujikimu
katika kipindi atakachokuwa nje ya uwanja.