![]() |
Yanga SC |
Na Princess Asia
KAMATI ya
Ligi imesogeza mbele kwa siku moja mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom kati ya Kagera
Sugar na Yanga iliyokuwa ichezwe kesho mjini Bukoba kutokana na Uwanja wa
Kaitaba kuwa na shughuli nyingine za kijamii.
Ofisa Habari
wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura Mgoyo ameiambia BIN ZUBEIRY
kwamba sasa mechi hiyo itachezwa Jumatatu kwenye Uwanja huo huo.
Wambura alisema
kwamba mabadiliko hayo pia yameathiri mechi kati ya Toto Africans na Yanga
iliyokuwa ichezwe Oktoba 10 mwaka huu Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza na sasa
itachezwa Oktoba 11 mwaka huu. Yanga tayari wapo Bukoba tangu asubuhi, baada ya
kuondoka Dar es Salaam kwa ndege.
Katika hatua
nyingine, Wambura amesema kwa vile msimu huu mdhamini mwenyewe ndiye anayegawa
vifaa kwa timu, Kamati ya Ligi imeagiza Vodacom iandikiwe barua na nakala kwa
klabu zote ili kujua timu ambazo tayari zimekabidhiwa vifaa hivyo zikiwemo logo
na siku ambapo timu husika zilipokea.
Baada ya
majibu ya Vodacom ndipo Kanuni za Ligi Kuu zitakapotumika kutoka adhabu kwa
timu ambazo zitabainika kuwa zilipokea vifaa lakini hazikuvitumia. Hatua hiyo
inafuatia timu za Yanga na African Lyon kutovaa jezi za wadhamini wa ligi hiyo
hadi sasa, kwa sababu mbalimbali.
Wakati Yanga
wanakataa nembo nyekundu kwenye jezi za wadhamini, Lyon wao wana mkataba wa
kampuni nyingine ya simu, Zantel.
Wakati huo
huo: Wambura amesema kwamba, Kamati ya Ligi ya TFF iliyokutana jana imepanga
Ligi Daraja la Kwanza (FDL), ianze kutimua vumbi Oktoba 20 mwaka huu.
Alisema timu
zimepangwa katika makundi matatu ya timu nane nane ambapo zitacheza ligi hiyo
kwa mtindo wa nyumbani na ugenini. Mshindi wa kila kundi ndiye atakayepata
tiketi ya kucheza Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) msimu ujao wakati timu ya mwisho
kila kundi itashuka daraja kurudi Ligi ya Mkoa.
Kundi A lina
timu za Burkina Moro ya Morogoro, Kurugenzi Mufindi ya Iringa, Majimaji ya Songea,
Mbeya City ya Mbeya, Mlale JKT ya Ruvuma, Mkamba Rangers ya Morogoro, Polisi
Iringa na Small Kids ya Rukwa.
Ndanda FC ya
Mtwara, Ashanti United, Green Warriors, Moro United, Polisi, Tessema, Transit
Camp na Villa Squad zote za Dar es Salaam ndizo zinazounda kundi B wakati kundi
C ni Kanembwa JKT ya Kigoma, Morani ya Manyara, Mwadui ya Shinyanga, Pamba ya
Mwanza Polisi Dodoma, Polisi Mara, Polisi Tabora na Rhino Rangers ya Tabora.
Ada ya
ushiriki wa ligi ni sh. 200,000 zinazotakiwa kulipwa kabla ya Oktoba 13 mwaka
huu. Pia Oktoba 13 mwaka huu kutakuwa na kikao kati ya wenyeviti wa klabu zote
zinazoshiriki ligi hiyo na Kamati ya Ligi ambapo pia itafanyika draw (ratiba).
0 comments:
Post a Comment