Na Princess Asia
KAMATI ya Uchaguzi ya Chama cha Soka kwa Wanawake Tanzania (TWFA) chini ya Mwenyekiti wake, Ombeni Zavala imewataka wanachama wa TWFA ambao ni mikoa ya Tanzania Bara kuwasilisha orodha ya wajumbe wao wa mkutano wa uchaguzi.
Wajumbe wenye sifa ya kuhudhuria Mkutano wa TWFA ni kutoka vyama vya mikoa ambavyo tayari vimefanya uchaguzi. Wajumbe hao ni Mwenyekiti, Katibu na Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TWFA.
Mikoa ambayo imeshafanya uchaguzi mpaka sasa ni Iringa, Kigoma, Mwanza, Pwani na Tanga. Mikoa ambayo bado inahimizwa kufanya uchaguzi, na mwisho wa kutuma majina ya wajumbe kwa Mwenyekiti Zavala ni Oktoba 25 mwaka huu.
Mkoa ambao utakuwa haujafanya uchaguzi utakuwa umenyimwa haki ya kushiriki uchaguzi wa TWFA utakaofanyika Novemba 4 mwaka huu.
Wakatin huo huo: Wambura amesema Chama cha Madaktari wa Tiba ya Michezo Tanzania (TASMA) leo kimetangaza kuanza mchakato wa uchaguzi wa chama hicho uliopangwa kufanyika Novemba 28 mwaka huu.
Kwa mujibu wa Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TASMA, Dk. Francis Mchomvu, fomu kwa wanamichezo wanaotaka kugombea uongozi wa chama hicho zitaanza kutolewa Oktoba 21 mwaka huu.
Mwisho wa kuchukua na kurejesha fomu hizo zinazopatikana ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ni saa 10.00 alasiri ya Oktoba 26 mwaka huu. Ada ya fomu kwa nafasi nne za juu ni sh. 200,000 wakati kwa nafasi nyingine zilizobaki ni sh. 100,000. Kati ya Oktoba 27-31 mwaka huu Kamati ya Uchaguzi ya TASMA itapitia fomu na kutangaza majina ya waliojitokeza kuomba uongozi.
Nafasi zitakazogombewa ni Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, Katibu Mkuu, Katibu Msaidizi, Mhazini, Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF na wajumbe wawili wa Kamati ya Utendaji.
Kipindi cha pingamizi kwa waombaji ni kuanzia Novemba 1-6 mwaka huu, na pingamizi zinatakiwa kuwasilishwa kwa Katibu wa Kamati ya Uchaguzi ya TASMA kabla ya saa 10.00 alasiri ya Novemba 6 mwaka huu. Hakuna ada kwenye pingamizi.
Pingamizi zitajadiliwa na kufanyiwa uamuzi kati ya Novemba 7-9 mwaka huu. Usaili utafanyika kati ya Novemba 10-11 mwaka huu ambapo matokeo ya usaili huo vilevile yatatangazwa ili kutoa fursa kwa rufani ambazo zinatakiwa kukatwa kati ya Novemba 11-13 mwaka huu.
Rufaa ambazo zinaambatana na ada y ash. 500,000 zinatakiwa kufikishwa kwa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kabla ya saa 10.00 alasiri ya Novemba 13 mwaka huu.