Twite alipowasili Uwanja wa Ndege kujiunga na Yanga Agosti mwaka huu |
Na Mahmoud Zubeiry
NI beki, lakini anawazidi washambuliaji kwa kufunga mabao.
Huyu ni Mbuyu Twite Banza, beki aliyesajiliwa msimu huu Yanga, kutoka APR ya
Rwanda, ambaye jana alifunga bao lake la tatu katika Ligi Kuu ya Vodacom
Tanzania Bara.
Pamoja na kufanya kazi nzuri ya ulinzi, akicheza beki ya kati
kwa pamoja na Nadir Haroub ‘Cannavaro’ katika kipindi hiki ambacho Kevin Yondan
anauguza goti aliloumizwa na Haruna Moshi ‘Boban’, Oktoba 3, mwaka huu, Twite
anasaidia sana na mashambulizi pia.
Hupanda kusaidia mashambulizi na kutoa pasi nzuri, lakini pia
huyo ndiye tegemeo la Yanga katika mipira ya adhabu hivi sasa.
Ana mashuti makali na ndiyo maana kocha Mholanzi, Ernie Brandts
ameamua kumfanya mtaalamu wake wa mipira iliyokufa.
Wakati Yanga wanafurahia matunda ya Twite, wazi wapinzani wao
wa jadi, Simba SC watakuwa wanaumia sana kumuona kijana huyo mwenye asili ya
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) akipiga mzigo wa uhakika Jangwani.
Kwa nini waumie? Simba SC ndio waliokuwa wa kwanza kumsajili
Twite baada ya michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la
Kagame- wakimtuma Mwenyekiti wao, Alhaj Ismail Aden Rage kwenda kukamilisha
usajili wake Kigali, Rwanda.
Rage alikutana na Twite, wakazungumza na kukubaliana, akampa
fedha dola za Kimarekani 30,000 na nyingine 1,000 kwa ajili ya tiketi ya kuja
Dar es Salaam. Rage alipogeuka tu, Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga,
Abdallah Ahmad Bin Kleb akamfuata Twite.
Bin Kleb akafanikiwa kumbadili mawazo Twite na kuamua
kurudisha fedha za Simba, ili aje Yanga, ingawa kidogo umafia ulitumika hapo.
Hadi leo Simba wanadai fedha zao walizompa Twite na tayari
TFF imeitaka Yanga irudishe fedha hizo.
Sahau kuhusu yote yaliyopita, kitu ambacho Yanga wanajivunia
kwa sasa ni kwamba, Mbuyu Twite ameanza kurudisha gharama zao za usajili.