Manji |
Na Mahmoud Zubeiry
MWENYEKITI wa Yanga, Yussuf Mehboob Manji anakwenda Mwanza
kuongeza morali ya wachezaji kwa ajili ya mechi ya kesho ya Ligi Kuu ya Vodacom
Tanzania Bara, dhidi ya wenyeji Toto Africans kwenye Uwanja wa CCM Kirumba kesho.
Habari kutoka ndani ya Yanga, ambazo BIN ZUBEIRY imezipata
zimesema kwamba Manji ameamua kwenda mwenyewe Mwanza, kufuatia timu kupoteza
mechi ya Bukoba juzi mbele ya wenyeji Kagera Sugar kwa kufungwa 1-0.
“Mwenyekiti anakwenda Mwanza, ili kwenda kuongeza morali ya
wachezaji, timu iweze kushinda mechi ya kesho,”kimesema chanzo chetu kutoka
Yanga ‘mida hii’.
Baada ya kufungwa na Kagera, Yanga wamedai wamegundua Simba
SC ‘wanatia mkono’ kwenye mechi zao na ndio maana zinakuwa ngumu, ila kuanzia
sasa na wao wanaanza ‘fitina’.
“Simba ilituma watu Bukoba watie mkono mechi yetu, sisi
tuliwashitukia hao watu baadaye sana, lakini tunashangaa kwa nini wanafanya hivi,
wakati sisi tulizungumza nao tukakubaliana haya mambo tuyaache, tucheze mpira,
sasa wao wanatuzunguka wanaendeleza mchezo mchafu,”alisema kiongozi Mjumbe
mmoja wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, ambaye hakutaka kutajwa jina.
Mjumbe huyo alisema kwamba wao walijua baada ya makubaliano
na Simba kutofanyiana fitina, waliamini mambo hayo hayatakuwapo, lakini baada
ya kugundua wenzao wamewageuka sasa na wao wanaanza ‘mchezo huo’.
“Na sisi sasa tunaanza kuzicheza mechi zao, wakumbuke tu wao
ndio walichokoza nyuki, sasa subirini kuanzia mechi yao na Coastal, wakishinda
wao wanaume, na pamoja na kuzicheza mechi zao, tunajizatiti katika mechi zetu.
Uzuri watu wote wanaowatumia tumekwishawajua, ni wale wale waliokuja Morogoro,
na wale wale waliokuja Bukoba. Tumekwishawajua,”alisema Mjumbe huyo.
Bao pekee la Themi Felix katika dakika ya 67, juzi liliwapa
Kagera Sugar ushindi wa 1-0 dhidi ya Yanga SC, kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba
katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Felix aliyeingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya
Mnigeria, Enyinna Darlington kwa kumtungua bao hilo, kipa Mghana wa Yanga, Yaw
Berko, ameendeleza rekodi yake kuvifunga vigogo, Simba na Yanga katika Uwanja
huo.
Hiyo inakuwa mechi ya pili Yanga kufungwa ndani ya mechi sita
walizocheza hadi sasa na mbili wametoka sare- maana yake inabaki na pointi zake
nane na kuzidi kujipunguzia matumaini ya ubingwa msimu huu, ikiwa sasa
inazidiwa pointi nane na vinara wa ligi hiyo Simba SC.
Aidha, hiyo ilikuwa ni mechi ya pili Yanga inacheza chini ya
kocha wake mpya, Mholanzi Ernie Blandts aliyerithi mikoba ya Mbelgiji, Tom
Saintfiet na katika mechi hizo mbili ameambulia pointi moja kutokana na sare
dhidi ya Simba Jumatano.
Kwa ujumla Yanga haijashinda hata mechi moja ya ugenini kati
ya tatu ilizocheza hadi sasa, ilitoka 0-0 na Prisons, ikafungwa 3-0 na Mtibwa
na jana imechapwa 1-0 na Kagera Sugar, wakati Alhamisi itacheza na Toto African
mjini Mwanza.
Katika mechi hiyo ya juzi, Yanga ilipata pigo dakika ya 23
baada ya mshambuliaji wake mahiri na tegemeo, Said Bahanuzi ‘Spider Man’
kuchanika nyama za paja dakika ya 23, baada ya kugongana na beki Benjamin Effe
wa Kagera Sugar na kushindwa kuendelea na mchezo, nafasi yake ikichukuliwa na
Jerry Tegete.
Tangu ajiunge na Yanga akitokea Mtibwa Sugar msimu huu, leo
Bahanuzi amecheza mechi ya 13 kwa dakika hizo 23 na ameifungia timu hiyo jumla
ya mabao 12, matatu kati ya hayo kwa penalti.