MAN UNITED YATAKA KUMRUDISHA BEKI WAKE ANAYETAKIWA PIA NA CHELSEA
Manchester United ina nia ya kumsajili tena beki wa kati, Ryan Shawcross, lakini itakabiliwa na ushindani kutoka kwa Chelsea na Tottenham. Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 25 alianzia soka Old Trafford kabla ya kuhamishiwa moja kwa moja Stoke mwaka 2008.
Juventus ina matumaini ya kuipiga bao Arsenal katika kuwania saini ya mshambuliaji wa Athletic Bilbao, Fernando Llorente kwa kutoa ofa kubwa ya kumnunua mpachika mabao huyo mwenye umri wa miaka 27.
Liverpool inatumai kumnasa winga wa Birmingham City, mwenye umri wa miaka 18, Nathan Redmond, kwa sababu mchezaji huyo wa timu ya taifa ya vijana ya England, aliyebakiza mwaka mmoja na nusu katika mkataba wake hafurahii maisha katika klabu hiyo ya Daraja la Kwanza kutokana na kutotimiziwa yaliyomo kwenye mkataba wake.
Kocha wa Everton, David Moyes bado hajaamua kumpa mkataba wa kudumu kiungo Thomas Hitzlsperger, mwenye umri wa miaka 30, ambaye amemvutia katika majaribio. Moyes pia hajaamua kumuongezea mkataba kiungo mwenye umri wa miaka 18, Ross Barkley anayecheza kwa mkopo Sheffield Wednesday.
Kocha wa Norwich, Chris Hughton anataka kumsajili mshambuliaji mwenye umri wa miaka 26 wa Stoke, Cameron Jerome.
Beki wa kati, Michael Dawson, mwenye umri wa miaka 28, anaamini bado ana maisha Tottenham, licha ya ukweli kwamba kocha Andre Villas-Boas alijaribu kumuuza msimu huu.
Kocha wa Newcastle, Alan Pardew ana orodha ya mabeki saba wa kati kuelekea usajili wa Januari na chaguo la kwanza ni Steven Taylor, mwenye umri wa miaka 26, na Fabricio Coloccini, mwenye miaka 30, ambao wote wamekuwa majeruhi msimu huu.
TERRY KUUZWA CHELSEA
Beki John Terry, mwenye umri wa miaka 31, ameambiwa atauzwa na Chelsea kama atakutwa na kashfa ya ubaguzi tena. Nahodha huyo wa zamani wa England, aliambiwa habari hiyo kwenye kikao cha bodi, kufuatia kushindwa kukata rufaa kwa kufungiwa mechi nne na Chama cha Soka kwa kutumia lugha ya kibaguzi.
Beki wa Manchester United, Rio Ferdinand, mwenye umri wa miaka 33, na mdogo wake mwenye umri wa miaka 27, Anton Ferdinand wa Queens Park Rangers watagoma kuvaa fulana za Kick It Out kutokana na oganazesheni hiyo kushindwa kuishawishi FA kutoa adhabu kali kwa matukio ya kibaguzi.
Liverpool itamkosa kipa wake Pepe Reina katika mechi ya Jumamosi dhidi ya Reading, baada ya mlinda mlango huyo mwenye umri wa miaka 30 kuumia nyama akiichezea Hispania.
Harry Redknapp, mwenye umri wa miaka 65, atarejea kwenye ukocha, iwapo tu atapata nafasi ya kuongoza klabu nyingine kubwa. .
Kiungo majeruhi wa Tottenham, Scott Parker, mwenye umri wa miaka 32, anaweza kuwa nje hadi Krisimasi akipambana kupona maumivu yake.
BALLACK AKAMATWA KWA KUENDESHA SPIDI 211
Kiungo Mjerumani wa zamani wa Chelsea, Michael Ballack, mwenye umri wa miaka 36, amekamatwa na Polisi nchini Hispania kwa kuendesha gari kwa mwendo kasi, wa spidi 211.