Deangelis Gabriel Barbosa akiwa na mkewe, Zaira Caroiline na mtoto wao, Lara Barbos. |
Mashaka Mhando, Tanga
KIUNGO mshambuliaji mpya wa Coastal Union anayetokea nchini
Brazili,Deangelis Gabriel Barbosa mwenye umri wa miaka 27, aliyetua Tanga
mwishoni mwa wiki na kuanza mazoezi na timu hiyo ameaahidi kuipa mafanikio ili
iweze kushiriki mashindano ya kimataifa barani Afrika.
Barbosa alitua jijini hapa akiwa pamoja na mke wake, Zaira
Caroline na mwanae Lara Barbos na ameahidi kuipa mafanikio timu hiyo kwa
kushirikiana na wachezaji wengine waliopo kwenye timu hiyo ambayo hivi sasa
inafanya vizuri katika mechi zao mbalimbali.
Katika mahojiano na mwandishi wa habari hizi, kiungo huyo amesema
anatokea Mtaa wa Bahia katika jiji la Paulo Afonso nchini Brazil na amesema atacheza
soka la kisasa kwa ajili ya kuipa heshima timu hiyo ndani na nje ya nchini kwa
kuwa anathamini mchezo huo ambao ni kazi yake.
Mchezaji huyo tayari ameanza mazoezi na wenzake na amesafiri
na timu hiyo ambayo leo inacheza na JKT Ruvu kwenye Uwanja wa Azam, Chamanzi,
Dar es Salaam ingawa hatacheza kwa sababu viongozi wa Coastal bado wanakamilisha
taratibu mbalimbali ikiwemo kibali chake cha kufanya kazi nchini.
Mchezaji huyo siku alipotambulishwa na Makamu Mwenyekiti wa
klabu hiyo, Steven Mgutto, alitaja timu mbalimbali alizochezea kuwa ni pamoja
na klabu ya New Road ya Nepal, ambako alipomaliza mkataba wake ndipo amekuja
Tanzania.
Mguto alisema wameingia mkataba wa miaka miwili na mchezaji
huyo na kueleza endapo kiwango chake kitakuwa kizuri watamuongezea mkataba mwingine.
Barbosa alisema atahakikisha anatoa mchango wake mkubwa
kwenye timu hiyo ili aweze kuipa heshima inayostahili ikiwemo kunyakua ubingwa
wa Ligi Kuu Tanzania Bara, ili timu hiyo iweze kushiriki mashindano makubwa.
Awali, Katibu wa Coastal Union, Kassim El Siagi aliwataka
wanachama pamoja na wapenzi wa timu hiyo, kuendeleza mshikamano uliopo ili
kuweza kutimiza malengo yao waliojiwekea ya kunyakua ubingwa wa Ligi Kuu msimu
huu.
Siagi alizitaja klabu ambazo mchezaji huyo aliwahi kuzicheza ni
Sports Club ya Paulo Afonso 2004, Maruinense Sporting Club 2006 za Brazil, Churuchill
Brothers ya India 2007-2008, Santa Cruz ya PB Brazili, 2009 Flamengo ya
Brazili, 2009-2010 Proham Football Club
ya Carribean na 2010 ya New Road Club ya Nepal.