Kiiza |
Na Mahmoud Zubeiry
HAMISI Friday
Kiiza maarufu Diego Milito, amerejea jana Dar es Salaam na leo anaingia
kambini, Uplands Hotel, Changanyikeni kuungana na wenzake kujiandaa na mchezo
wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Ruvu Shooting Jumamosi wiki hii
kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kiiza alikuwa Uganda, kuichezea timu yake ya taifa, The
Cranes katika mchezo wa marudiano wa kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Kombe
la Mataifa ya Afrika mwakani nchini Afrika Kusini.
Uganda ilitolewa na Zambia kwa mikwaju ya penalti baada ya
sare ya jumla ya 1-1, Zambia wakianza kushinda nyumbani 1-0 na Uganda wakashinda
kwao 1-0 pia mwishoni mwa wiki, hivyo mchezo kuhamia kwenye mikwaju ya penalti,
ambako timu ya Kiiza ilitolewa.
Pamoja na kuweka kambi Changanyikeni, lakini Yanga inafanya
mazoezi kwenye Uwanja wa shule ya sekondari ya Loyola, Mabibo, Dar es Salaam.
Beki Kevin Yondan aliyeumizwa na kiungo wa Simba, Haruna
Moshi ‘Boban’ katika mechi baina ya wapinzani hao wa jadi, Oktoba 3, mwaka huu,
anaendelea vizuri na mazoezi mepesi sawa na mshambuliaji Said Bahanuzi
aliyekuwa anasumbuliwa na maumivu ya nyama za paja.
Bahanuzi
‘Spider Man’ alichanika nyama za paja la mguu wa kulia katika mechi ya Ligi Kuu
ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba
Jumatatu wiki iliyopita.
Bahanuzi
aliumia dakika ya 23, baada ya kugongana na beki Benjamin Effe wa Kagera Sugar
na kushindwa kuendelea na mchezo, nafasi yake ikichukuliwa na Jerry Tegete
katika mechi ambayo Yanga ililala 1-0, beo pekee la Themi Felix.
Bahanuzi
ndiye tegemeo la mabao la Yanga kwa sasa, kwani tangu ajiunge na timu hiyo
akitokea Mtibwa Sugar msimu huu, ameifungia mabao 12 katika mechi 13, ikiwemo
ile dhidi ya Kagera aliyocheza kwa dakika 23 kabla ya kuumia na kutoka.
Yanga kwa
sasa inashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu kwa pointi zake 11,
baada ya kucheza saba, kushinda tatu, sare mbili na kufungwa mbili.
Simba
iliyocheza mechi nane, inaongoza ligi hiyo kwa pointi zake 18, ikifuatiwa na
Azam FC yenye pointi 17, iliyocheza mechi saba.