Boniface Wambura |
Na Princess Asia
OFISA Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface
Wambura ameteuliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kuwa mmoja wa maofisa
watakaoshughulikia masuala ya habari wakati wa Fainali za Mataifa ya Afrika kwa
Wanawake zitakazofanyika nchini Equatorial Guinea.
Uteuzi huo umefanywa na Rais wa CAF, Issa Hayatou kwa ajili
ya kufanikisha uendeshaji wa fainali hizo za Mataifa ya Afrika kwa Wanawake
zilizopangwa kuanza Oktoba 28, 2012 na kumalizika Novemba 11, 2012.
Wambura atakuwa mmoja wa maofisa watatu watakaoshughulikia
habari kwenye fainali hizo. Wengine ni ofisa kutoka makao makuu ya CAF, Mahmoud
Garga na Arlindo Macedo kutoka Angola.
Wambura atakuwa ni Mtanzania pekee kwenye Kamati ya
Maandalizi ya fainali hizo, kitu ambacho TFF inajivunia kutoa mwakilishi kwenye
moja ya mashindanoi makubwa ya mpira wa miguu Tanzania.
Rais wa TFF, Leodegar Tenga ameelezea uteuzi huyo kuwa ni matokeo ya kazi nzuri ambayo
Wambura amekuwa akiifanya tangu ajiunge na Shirikisho Januari mwaka 2011.
“Taarifa zake mbalimbali zimeifanya Tanzania iwe inang’ara
CAF na hata FIFA kwa kuwa kwa sasa wanajua kila kinachoendelea kwenye soka la
Tanzania,” alisema Rais Tenga na kumtakia Wambura kila la kheri kwenye kazi
hiyo atakayoifanya kwa takriban siku 14.
Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah, akizungumza kwa niaba ya
Sekretarieti, amemtakia Wambura kazi njema na kwamba awe kioo cha mabadiliko
makubwa yanayoendelea kwenye soka la Tanzania.
Wambura alijiunga na TFF Januari, 2011 akiwa mmoja wa
waajiriwa watatu wapya kwenye Shirikisho baada ya wsatendajiu wengine wawili
kumaliza muda wao wa mikataba.
Wambura ni mwandishi wa habari mwandamizi ambaye ameshafanya
kazi kwenye vyombo mbalimbali kuanzia kazi ya uandishi hadi Mhariri Mtendaji wa
gazeti la Jambo Leo ambalo alikuwa akifanya kazi kabla ya kujiunga na TFF.