Kavumbangu |
Na Mahmoud Zubeiry
DIDIER Fortine Kavumbagu yuko fiti kuichezea klabu yake,
Yanga SC katika mechi ya kesho ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Mgambo
JKT, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mrundi huyo alivimba mguu baada ya mechi dhidi ya JKT Oljoro
na kushindwa kufanya mazoezi jana, lakini amefanya mazoezi na kumpa moyo kocha
Mholanzi, Ernie Brandts kwamba anaweza kutumika kesho.
Beki Kevin Patrick Yondan na mshambuliaji Said Rashid
Bahanuzi nao wapo fiti kabisa na leo pia wamefanya mazoezi na wenzao kwa ukamilifu
Uwanja wa sekondari ya Loyola, Mabibo, Dar es Salaam.
Kipa Said Mohamed Kasarama na kiungo Juma Seif Dion ‘Kijiko’
wanasumbuliwa na Malaria na hawatashiriki mechi hiyo ya kesho, wakati mabeki
Salum Abdul Telela, Juma Jaffar Abdul na Ibrahim Job Isaac wote bado majeruhi.
Yanga iliyovuna pointi tatu kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya JKT
Oljoro, Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha na kupanda nafasi ya pili kwenye
msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, baada ya kutimiza pointi 20 katika
mechi 10, kesho inatarajiwa kuendeleza mawindo yake.
Yanga sasa iko nyuma kabisa ya wapinzani wao wa jadi, Simba
SC wanaoongoza Ligi Kuu kwa pointi zao 22, baada ya kucheza mechi 10 pia.
Mabingwa hao wa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame,
wanaweza kupanda kileleni kesho, iwapo Simba itatoa sare au kufungwa na Polisi
mjini Morogoro katika mchezo mwingine wa Ligi Kuu.
Mgambo JKT pamoja na kwamba imepanda Ligi Kuu msimu huu,
lakini imeonyesha ni timu ya ushindani baada ya kutoa sare ya bila kufungana na
Simba SC, Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
Kwa sababu hiyo, Yanga wamechukua tahadhari ya kutosha
kuelekea mchezo huo na tangu juzi Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga,
Abdallah Ahmad Bin Kleb amekuwa ‘akienda mbio’ kuhakikisha timu inashinda
keshokutwa.
Kurejea kwa Yondan na Bahanuzi kunaongeza matumaini ya
ushindi kwa Yanga katika mchezo huo, ingawa upande mwingine ni mtihani kwa
Brandts, kwani katika kipindi ambacho wachezaji hao wako ‘wadini’, walioshika
nafasi zao wamekuwa wakifanya vizuri.
Mbuyu Twitwe aliyehamishwa kutoka beki ya kulia hadi beki ya
kati tangu Yondan aumie Oktoba 3, amekuwa akifanya vizuri sawa na Jerry Tegete
aliyempokea Bahanuzi Oktoba 8, alipoumia naye amekuwa akifanya vizuri pia.
Kwa kuzingatia Twite alikuwa ‘uchochoro’ alipokuwa akicheza
pembeni, watu wanasubiri kuona kama Brandts atamrudisha huko huko baada ya
Yondan kurejea, au ataamua mmoja kati yao na Nadir Haroub ‘Cannavaro’ ataanzia
benchi.
Upande wa Tegete na Bahanuzi, kuna uwezekano mmoja wao
atakuwa anaanzia benchi kwa sasa na mwingine kumpokea mwenzake baadaye.