Alex Mgongolwa |
Na Mahmoud Zubeiry
MWENYEKITI wa Kamati ya Sheria,
Maadili na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wakili Alex
Mgongolwa amesema kwamba Kamati yake itakutana tena hivi karibuni, kujadili
hatua za kuichukulia klabu ya Yanga kwa kukaidi agizo la kuilipa Simba SC fedha
alizochukua mchezaji wao, Mbuyu Twite dola za Kimarekani 32,000.
Akizungumza na BIN ZUBEIRY ‘mida hii’,
Mgongolwa alisema kwamba tayari amekwishamuagiza Katibu wa TFF, Angetile Osiah
aitishe kikao cha Kamati hiyo, kujadili zaidi sakata hilo.
“Tutakutana kujadili na kuamua
hatua za kuchukua, unajua maamuzi ya awali ya Kamati, yalikuwa Yanga walipe
hizo fedha hadi kufika Oktoba 3, lakini kwa kuwa wameshindwa kufanya hivyo,
inabidi Kamati ikutane tena kujadili hatua za kuchukua.
Ndiyo maana hata wale waliotaka
Yanga wakatwe fedha hizo katika mapato yao ya milangoni, ilishindikana kwa kuwa
hayo hayakuwa maamuzi ya Kamati yetu,”alisema Mgongolwa.
Septemba 10, mwaka huu Kamati ya
Sheria na Hadhi za Wachezaji, iliitaka Yanga kulipa dola 32,000 za Simba alizochukua
Twite ndani ya 21, ambazo ziliisha Oktoba 3, mwaka huu.
Hatua hiyo, ilifuatia baada ya
Twite kusaini Simba na baadaye kuikana klabu hiyo na kusaini Yanga aliyojiunga
nayo.
Wajumbe sita kati ya saba waliopo
walihudhuria kikao hicho chini ya Mwenyekiti Alex Mgongolwa. Wajumbe hao ni
Hussein Mwamba, Imani Madega, Ismail Aden Rage, Llyod Nchunga na Omari Gumbo.
Ikumbukwe kesi ya msingi ilikuwa ni malalamiko ya Simba kufanyiwa mchezo usio wa kiungwana na watani wao hao wa jadi, Yanga kwa kuingilia usajili wao kwa Twite na kumsaini beki huyo wakati tayari amekwishaingia mkataba na Simba.