KAMA ilivyotarajiwa na wengi, refa Mathew Akrama wa Mwanza
aliyechezesha ovyo mechi ya watani wa jadi katika soka ya Tanzania, Simba na
Yanga, Jumatano wiki hii Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ‘amekwenda na
maji’.
![]() |
| Na Mahmoud Zubeiry |
Mbali na Akrama, mwamuzi msaidizi namba mbili wa mechi hiyo ya Yanga na
Simba, Ephrony Ndissa wa Dar es Salaam naye amepewa onyo.
Huyu si refa wa kwanza aliyechezesha mechi ya wapinzani wa jadi
kufungiwa baada ya mchezo na tathmini inaonyesaha asilimia 70 ya marefa wa
mechi hizo katika kipindi cha muongo mmoja uliopita wamekuwa wakifungiwa.
Wanafungiwa kwa sababu wanashindwa kuzimudu hizo mechi, iwe kwa utashi,
ushawishi au uwezo mdogo, ukweli unabaki pale pale, wanashindwa kuzimudu mechi
hizo kulingana na uzito wake.
Wachambuzi na watangazaji wa SuperSport waliwahi kuiingiza mechi ya
Simba na Yanga katika orodha ya mechi tatu kali za wapinzani wa jadi Afrika -
nyingine zikiwa ni kati ya Orlando Pirates na Kaizer Chiefs za Afrika Kusini na
Al Ahly dhidi ya Zamalek za Misri.
Lakini mimi naongeza mechi ya wapinzani wa Ghana, Hearts Of Oak na
Asante Kotoko, ingawa Kenya nako upinzani wa Gor Mahia na AFC Leopard umeanza
kuja juu tena, baada ya kuporomoka miaka ya karibuni, kutokana na kuyumba kwa
timu zenyewe.
Hakuna ubishi upinzani wa Ahly na Zamalek huo ni dunia nzima - ni zaidi
ya upinzani, lakini kwa Afrika fuatilia ligi nyingi, utagundua Simba na Yanga
ni mechi yenye mvuto wa kipekee na ndiyo maana hivi sasa SuperSport wamekuwa
wakionyesha mfululizo mechi za watani hao, ingawa hawana mkataba na Shirikisho
la Soka Tanzania (TFF) wa kuonyesha mechi za Ligi Kuu.
Unaweza kutilia shaka kiwango cha soka cha timu hizo, lakini si
upinzani wao kwa maana ya upinzani. Upinzani wao ni sehemu ya burudani na kama
iko siku zitakuwa imara na kucheza soka ya kuvutia, basi burudani itakuwa mara
mbili.
Hata hivyo kuna mambo mawili au matatu ambayo kwa kiasi fulani yamekuwa
yakipunguza ladha ya mechi za watani hao wa jadi.
![]() |
| Akrama; Hatutamuona tena Ligi Kuu |
Awali tatizo kubwa lilikuwa Uwanja mdogo wa Uhuru, lakini tangu
kukamilika kwa Uwanja wa Taifa ambao tumeshuhudia mechi zote zilizochezwa hapo,
haijatokea mechi hata moja mashabiki wakajaza viti, mambo yamekuwa mazuri.
Matatizo mawili yaliyobakia ni viwango vya timu kuboreshwa, ili ifike
wakati pamoja na upinzani, kukamiana lakini watazamaji washuhudie soka safi.
Tatizo la pili ni marefa, kweli ilipofikia na kama kweli lengo ni
kuiongezea msisimko zaidi mechi ya watani, waamuzi wa Tanzania wawekwe kando na
watumike waamuzi kutoka nje ya nchi, tena ikibidi nje kabisa ya nchi tatu za
Jumuiya yetu ya Afrika Mashariki.
Rejea mchezo wa Jumatano, yule refa Akrama huwezi kujua umuweke katika
kundi lipi, utashi wake, ushawishi au uwezo mdogo kulingana na ukubwa wa mechi-
lakini jibu moja tu alichemsha.
Rafu ambayo Haruna Moshi ‘Boban’ alimchezea Kevin Yondan, siyo tu
ilikuwa rafu mbaya kuliko zote katika mechi hiyo, bali rafu mbaya zaidi tangu
kuanza kwa Ligi Kuu katika mechi zilizochezwa mbele ya macho yangu.
Nasema mbele ya macho yangu kwa sababu kuna mechi zilinipita zilizochezwa
nje ya Uwanja wa Taifa, lakini pia kulingana na taarifa za vyanzo, vikiwemo vyombo
vya habari rafu ya Boban kwa Yondan inaweza kuwa ndio rafu mbaya zaidi hadi
sasa katika msimu huu wa Ligi Kuu.
Tuweke unazi pembeni, Akrama aliharibu mno ule mchezo, ila kwangu bado
anakuwa na nafuu kuliko yule refa wa Mei 6, 2012, aliyetoa penalti tatu na kadi
moja nyekundu kwa Yanga, ikichapwa 5-0 na Simba.
Hii si sahihi katika mechi za wapinzani wa jadi, dhahiri refa huyu
alishindwa kuumudu mchezo wa watani hata kama alifuata sheria 17. Katika mechi
ya wapinzani wa jadi, ukishatoa kadi moja nyekundu kwa timu moja, unajifikiria
sana kurudia kutoa kadi ya pili kwa timu hiyo hiyo.
Katika mechi za wapinzani wa jadi, ukishatoa penalti moja kwa timu
moja, unajifikiria sana kutoa penalti ya pili kwa timu hiyo hiyo. Unafikiria
mengi. Tena mengi sana.
Rejea mechi ya Machi 5, mwaka 2011 Uwanja wa Taifa, refa Orden Mbaga
aliivuruga mno mechi hiyo, kutokana tu na pengine mchecheto ama kutaka kufanya
kile ambacho kinaitwa ‘kubalansi’ mchezo au kukwepa lawama, matokeo yake
anafanya madudu.
Dakika ya 58 Juma Said Nyosso alimkwatua Davies Robby Mwape kwenye eneo
la hatari akawapa penalti Yanga na kilichofuatia wengi walijua beki huyo wa
Simba atatolewa nje kwa kadi nyekundu, badala yake akampa kadi ya njano.
Ngumu kuamini Mbaga, refa mwenye beji ya Shrikisho la Soka la Kimataifa
(FIFA) hajui alipaswa kufanya nini kwa Nyosso, lakini kwa sababu ni refa wa
nyumbani na aliongoza wapinzani wa jadi katika mechi ya nyumbani, alihofia
kumtoa mchezaji kwa kadi nyekundu angeshushiwa lawama nzito. Marefa hufanyiwa
fujo na kupigwa na mashabiki, labda alihofia hali hiyo pia.
Dakika ya 73 Simba walipata bao safi la kusawazisha lililofungwa kwa
kichwa na Mussa Hassan Mgosi, aliyeuwahi mpira uliotemwa na kipa Yaw Berko kufuatia shuti la mpira wa adhabu,
lililogonga mwamba wa juu na kudondokea nyavuni kabla ya kuokolewa na mabeki wa
Yanga.
Halikuwa bao lenye shaka yoyote, hakukuwa na kuotea wala dosari yoyote,
lakini haieleweki kwa nini Mbaga alilikataa bao hilo awali.
Ilikuwa offside au mpira haukutinga nyavuni hadi akalikataa kwanza?
Haijulikani, lakini alilikubali baada ya wachezaji wa Simba kumuambia aangalie
kwenye TV iliyokuwapo uwanjani marudio ya tukio lile na baada ya hapo akaenda
kujadiliana na msaidizi wake, ndipo akalikubali.
Mbaga alichemsha- lakini si Mbaga tu, marefa wengi wa Tanzania waliwahi
kutokota kabla yake na nitakumbushia baadhi ya mechi.
Machi 31, mwaka 2002 katika fainali ya Kombe la Tusker, Simba ikishinda
4-1, refa Abdulkadir Omar ‘Msomali’ aliivuruga mechi na kuvuruga amani uwanjani
pia kwa madudu yake.
Kwa nini? Katika mechi hiyo ya fainali iliyohudhuriwa na rais mstaafu
wa awamu ya pili ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi,
chupuchupu ivunjike dakika ya 32, baada ya Madaraka Suleiman kufunga bao ambalo
kabla ya kufumua shuti lililomshinda kipa Manyika Peter, aliushika mpira kwa
makusudi, ili kuuweka sawa.
Rais wa Yanga wakati huo, Tarimba Abbas aliinuka na kuwaonyesha ishara
wachezaji wake watoke uwanjani na hapo ndipo meza kuu aliyokuwa ameketi mzee
Mwinyi, ilipoanza kushambuliwa kwa chupa za maji na mashabiki wa Yanga.
Abdulkadir Omar alisubiri hadi vurugu zilipotulizwa na FFU ndipo akaendeleza
mchezo. Tarimba alitoka nje na hakutaka kuendelea kushuhudia mchezo huo. Baada
ya hapo, alifungiwa na Chama cha Soka Tanzania, (FAT), sasa TFF kabla ya
kujiuzulu uongozi wa klabu hiyo baadaye.
Agosti 18, mwaka 2002 Simba na Yanga zikitoka sare ya 1-1 katika mechi
ya Ligi Kuu, refa Victor Mwandike aliwaacha mashabiki wa Simba midomo wazi kwa
kuwapa Yanga penalti dakika ya 89 na ushehe, ambayo Sekilojo Chambua aliitumia
vema kuisawazishia bao timu yake, baada ya Simba kutangulia kufunga kupitia kwa
Madaraka Suleiman dakika ya 65.
Oktoba 24, mwaka 2007, refa Osman Kazi alikataa mabao matatu
yaliyofungwa na Yanga, yote akidai kipa Juma Kaseja alisukumwa na wachezaji wa
Yanga, lakini kwa yeyote atakayerudia kuangalia DVD ya mchezo ule, hawezi kuona
ukweli wa madai ya Kazi.
Awali ya hapo, Kazi aliwahi kupuliza filimbi ya kumaliza dakika 45 za
kipindi cha kwanza katika Nusu Fainali ya Kombe la Tusker mwaka 2005 mjini
Mwanza, wakati mchezaji wa Yanga, Said Maulid ‘SMG’ amekwishawatoka mabeki wa
Simba na anakwenda na mpira mbele yake amebaki Juma Kaseja tu.
Refa ni mwamuzi wa mwisho- lakini kwa wana Yanga walijutia mno tukio
lile kwenye mchezo ambao mwishowe walifungwa 2-0, kwa mabao ya kipindi cha pili
ya Emmanuel Gabriel na Mussa Mgosi.
Aprili 19, mwaka 2009, Jerry
Tegete aliifungia Yanga bao la kusawazisha kwa mkono na kutengeneza sare ya
2-2, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Refa makini asingeweza kukubali bao lile,
hivyo kwa haya yote lazima tukubali marefa wa Tanzania hawawezi tena kuchezesha
mechi za watani wa jadi.
Sababu nyingine za marefa wetu kuzishindwa mechi hizo ni mapenzi yao
kwa moja ya timu hizo, kitu ambacho Misri wamekiepuka na mechi ya Zamalek na
Ahly inachezeshwa na marefa kutoka nje ya nchi yao.
Nakumbuka refa kutoka Uganda, Dennis Bate aliyechezesha Nusu Fainali ya
Kombe la Tusker mwaka 2009 kati ya Simba na Yanga, aliiongoza vizuri mechi hiyo
na akadhibiti ujanja wote wa wachezaji kutaka kumdanganya na hatimaye aboronge.
Kuna wachezaji wanaitwa wazoefu wa mechi za Simba na Yanga na hawa
wamekuwa wakiwapoteza sana marefa kwa uzoefu wa kucheza mechi hizo, lakini kama
marefa watatoka nje ya Tanzania, tena wa kiwango cha beji za FIFA, uhondo wa
mechi za watani utaongezeka maradufu.
Kabla ya mchezo wa Jumatano niliandika juu ya mechi za watani wa jadi
kubadilishiwa marefa, ikiwa ni marudio- lakini wakubwa wameendelea kukaa kimya
na wanaona kuwafungia marefa ndio tiba.
Siyo tiba- zaidi ni kuwanyanyasa, kwa sababu hoja ya msingi hapa ni
kwamba hii mechi iko nje ya uwezo wao marefa wa Tanzania- iwe wanavuruga kwa
utashi wao, huwezi kuuzuia, ushawishi huwezo kupambana nao na kama ni uwezo
mdogo hilo ndilo haliwezekani kabisa kuligeuza mara moja.
Wamisri si wajinga kuamua mechi yao ya wapinzani wa jadi ichezeshwe na
marefa kutoka nje na sioni sisi ni
weledi kiasi gani hata hatutaki kuiga mbinu zuri namna hii ya kuilinda hii
mechi ya wapinzani, ambayo ndio pekee imebaki inaubeba msisimko wa soka ya
Tanzania.
Itapendeza sana, Simba na Yanga refa wanamjua TFF tu, kama mechi
Jumamosi anafika Ijumaa anapiga kazi Jumamosi, Jumapili anaondoka. Huyu anakuja
kutoka huko, hana mapenzi na timu yoyote, lazima atafanya vizuri tofauti na
marefa wetu ambao kila mechi ikipita wanafutwa.




.png)
0 comments:
Post a Comment