Kiemba aliyeruka juu kufunga bao la pili la Simba jana kwa krosi ya Nassor Masoud 'Chollo' |
Na Mahmoud Zubeiry
KATIKA mechi
zote za mwanzo, Profesa Milovan Cirkovick amekuwa akimpanga Amri Kiemba kama
kiungo mkabaji, lakini kuanzia mechi na Yanga Jumatano iliyopita, amefanya
mabadiliko kidogo kwenye kikosi chake.
Amekuwa akimpanga
Jonas Mkude kama kiungo mkabaji na mbele yake anakuwapo Mwinyi Kazimoto na viungo
wote wa pembeni wanakuwapo kama kawaida.
Ila, utaona
Simba inaanza na mshambuliaji mmoja tu, Felix Sunzu pekee, lakini inakuwa na
kiungo mmoja wa ziada uwanjani, ambaye anafahamika kama kiungo mkabaji.
Huyo ni Amri
Kiemba. Tangu mechi hiyo, Kiemba amekuwa kama mchezaji huru uwanjani. Anafika maeneo
yote. Anasaidia vema, tena sana ulinzi- anasaidia vizuri, tena mno kuiendesha
timu. Anasaidia kwa kiasi kikubwa mashambulizi.
Kiemba akishangilia baada ya kufunga baio la tatu ndani ya mechi mbili |
Profesa Milovan |
Katika mechi
hizo mbili, Kiemba amefunga mabao matatu, moja dhidi ya Yanga na mawili jana
dhidi ya JKT Oljoro, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Jana Kiemba angeweza
kushangaza watu kwa kufunga mabao matatu, kwani kuna bao moja la wazi sana
alikosa kipindi cha pili.
Tazama ni
wakati gani Kiemba huwa anafunga kwa kurejea mabao yake yote matatu- utaona ni
kutokana na mashambulizi yale ya haraka kuanzia nyuma upande wao- maana yake
anakwenda vema mwelekeo wa shambulizi.
Hili linakuwa
shambulizi ambalo limepangwa kutokana na maelekezo ya kocha wao, na kwa sababu
mabeki wengi kwenye mipira inayotokea pembeni huwamulika zaidi washambuliaji,
basi vivyo hivyo Sunzu ndiye amekuwa akiwekewa ulinzi mkali, Kiemba anamaliza
kazi.
Hii sasa
inaanza kutupa picha kwa nini marehemu Patrick Mafisango pamoja na kuwa kiungo,
msimu uliopita alikuwa mfungaji bora wa Simba kwa mabao yake 10, mbele ya
washambuliaji hodari kama Emanuel Okwi na Sunzu.
Hapa unaweza
kuona kocha anafanya kazi gani katika timu. Hapa unaweza kutofautisha kocha na
msimamizi wa mazoezi. Milovan ni kocha.