Blandts kushoto akiwanoa wachezaji wake, leo watashinda Mwanza? |
Na Mahmoud Zubeiry
MABINGWA wa kihistoria wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara,
Yanga SC ya Dar es Salaam, leo wanashuka kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza
kumenyana na wenyeji Toto African, katika mchezo ambao wamepania kushinda ili
kurejesha matumaini ya kutwaa ubingwa msimu huu.
Yanga ambayo katika mechi sita ilizocheza hadi sasa,
imefungwa mbili, sare mbili na kushinda mbili, inazidiwa pointi nane na
wapinzani wake wa jadi, Simba SC wanaoongoza ligi hiyo kwa pointi zao 16,
wakifuatiwa na Azam.
Msimu uliopita, Yanga iliambulia nafasi ya tatu katika Ligi
Kuu na kukosa nafasi ya kucheza michuano ya Afrika, Simba walioibuka mabingwa wakijikatia
tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa na washindi wa pili Azam watashiriki Kombe
la Shikrikisho.
Na tayari sasa Yanga wameanza kuhofia hali hiyo kujirudia na msimu
huu, hivyo wameamua kukaza uzi, ili kujihadhari na matokeo mabaya.
Baada ya kufungwa mechi iliyopita na Kagera Sugar mjini
Bukoba, Yanga wamepania kushinda leo na inaelezwa hadi Mwenyekiti wake, Yussuf
Mehboob Manji amekwenda Mwanza kuongeza morali ya wachezaji kwa ajili ya mechi hiyo.
Kihistoria, Toto ni tawi la Yanga pale Mwanza, lakini
uhusiano wao unaonekana kuanza kuyumba, baada ya timu hiyo ya Kishamapanda
kuwageuzia kibao baba zao msimu uliopita kwa kuwafunga katika mchezo ambao
walihitaji kushinda ili kufukuzana na Simba na Azam.
Tayari kuna imani ndani ya Yanga kwamba wapinzani wao, Simba
SC ‘wanatia mkono’ mechi zao kwa kuzipa motisha timu wanazocheza nazo zicheze kwa
nguvu na kwamba hiyo ndiyo inasababisha mechi zao zinakuwa ngumu msimu huu.
Na ni kwa sababu hiyo katika mchezo wa leo, matajiri wote wa
Yanga watakuwapo kwenye Uwanja wa Kirumba kuhakikisha baada ya dakika 90
wanaondoka na pointi tatu.
Mechi ya leo itakuwa ya tatu Yanga inacheza chini ya kocha wake
mpya, Ernie Blandts ambaye hadi sasa hajashinda hata mechi moja, akiwa ametoa
sare moja na wapinzani wao wa jadi, Simba SC, kufungwa moja dhidi ya Kagera.
Katika mchezo wa leo, Yanga itawakosa wachezaji wake wanne wa
kikosi cha kwanza, beki Kevin Yondan, mshambuliaji Said Bahanuzi ambao wote ni
majeruhi waliomua katika mechi mbili zilizopita, mshambuliaji Hamisi Kiiza
aliyerejea kwao Uganda kuchezea timu yake ya taifa na kiungo Simon Msuva
anayetumikia adhabu ya kadi.
Yondan alikanyagwa na Haruna Moshi ‘Boban’ kwenye mechi dhidi
ya Simba Jumatano iliyopita Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na atakuwa nje kwa
wiki mbili na ushei, wakati Bahanuzi aliumizwa na Benjamin Effe wa Kagera Jumatatu
naye atakaa nje kwa wiki moja au zaidi.
Lakini bado Blandts, beki wa zamani wa kimataifa wa Uholanzi,
aliyeng’ara kwenye Fainali za Kombe la Dunia mwaka 1978 ana wachezaji wengine
wa ushindi, ambao anaweza kuwatumia leo.
Bila shaka, kikosi Yanga leo kitakuwa; Yaw Berko, Juma Abdul,
Stefano Mwasyika, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Mbuyu Twite, Athumani Iddi ‘Chuji’,
Frank Domayo, Nizar Khalfan, Didier Kavumbangu, Jerry Tegete na Haruna
Niyonzima.
Katika mechi ya jana ya ligi hiyo, Kagera Sugar walilazimishwa
sare ya bila kufungana na JKT Ruvu ya Pwani katika mchezo uliofanyika kwenye
Uwanja wa Kaitaba, Bukoba.