John Bocco akiwa chini ya benchi la Azam baada ya kuumia. |
ILITARAJIWA kuwa mechi ngumu na hata ilivyoanza ilionekana
itakuwa mechi ngumu, lakini ndani ya dakika 22 mwelekeo mzima ukabadilika.
Na Mahmoud Zubeiry |
Naizungumzia mechi ya jana ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania
Bara, baina ya mabingwa watetezi, Simba SC dhidi ya washindi wa pili wa ligi
hiyo msimu uliopita, Azam FC.
Katika mechi hiyo, iliyopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam,
Simba ilitoka nyuma kwa bao 1-0 na kushinda 3-1.
Ushindi huo, unaifanya Simba izidi kujitanua kileleni mwa ligi
hiyo kwa kufikisha pointi 22, baada ya kucheza mechi 10, wakati Azam FC
inapromoka hadi nafasi ya tatu kwa pointi zake 18, baada ya kucheza mechi tisa,
ikiipisha Yanga nafasi ya pili, ambayo imetimiza pointi 20 baada ya kuifunga
JKT Oljoro jana.
Mabao ya Simba jana yalitiwa kimiani na Emanuel Arnold Okwi
mawili na Felix Mumba Sunzu Jr. moja, wakati la Azam lilifungwa na John Raphael
Bocco ‘Adebayor’.
Hadi mapumziko, tayari Simba walikuwa mbele kwa mabao 2-1,
Azam wakitangulia kufunga dakika ya nne, kupitia kwa Adebayor ambaye alimtoka
beki Mkenya Paschal Ochieng na kumchambua Juma Kaseja.
Dakika mbili baadaye, Sunzu aliisawazishia Simba,
akiunganisha kwa kichwa krosi maridadi ya Mrisho Khalfan Ngassa kutoka wingi ya
kulia.
Okwi aliifungia Simba bao la pili kwa kichwa dakika ya 40,
baada ya kutokea kizaazaa langoni mwa Azam kufuatia mpira uliopigwa langoni mwa
timu hiyo na Mwinyi Kazimoto.
Kipindi cha pili Simba walirudi na moto wao na iliwachukua
dakika tano tu kuhitimisha karamu yao ya mabao, baada ya Okwi kuwainua tena
vitini mashabiki wa Simba, akifumua shuti la umbali wa mita 19, baada ya
kuwatoka mabeki wa Azam.
Mrisho Ngassa ndiye alikuwa nyota wa mchezo wa jana, kutokana
na kuisumbua mno Azam, iliyomuuza kwa mkopo Simba miezi miwili iliyopita.
Kulingana na kuporomoka kwa kiwango cha soka yetu, kwa sasa mechi
za uhakika zilizobaki ambazo unaweza kuziita za ushindani ni kati ya Simba na Azam,
Simba na Yanga na Yanga na Azam.
Zipo timu nyingine ambazo zinaleta ushindani, lakini si wa
uhakika sana- ila Azam, hakika imeleta changamoto mpya katika soka ya Tanzania.
Mechi ya jana Simba walishinda kwa urahisi pengine tofauti
kabisa na wao walivyotarajia. Simba walitarajia ugumu mno kwenye mechi hiyo
hata wakaamua kwenda kuweka kambi Zanzibar kujiandaa vizuri.
Waliipa mechi hiyo uzito wa mechi zao na Yanga ndiyo maana
wakaenda Zanzibar, ambako tumezoea kusikia Simba ikienda katikati ya Ligi, basi
kwa ajili ya kucheza na wapinzani wao hao wa jadi.
Kwa nini mechi ilikuwa nyepesi ghafla?
Mfungaji wa bao la kwanza katika mechi hiyo, John Bocco ‘Adebayor’
aliumia dakika ya 20 na jitihada za kumtibu kwa dakika nne zilishindikana
hatimaye akatoka na nafasi yake ikachukuliwa na kiungo Khamis Mcha ‘Vialli’
dakika ya 25.
Hapo ndipo mechi ilipobadilika kabisa, kwa sababu kuanzia
hapo Azam ilicheza bila mshambuliaji uwanjani.
Sijui kwa sababu gani kocha Mserbia wa Azam, Boris Bunjak na
wasaidizi wake walishindwa kuingiza mshambuliaji mwingine baada ya kuumia Bocco
na badala yake wakaingiza kiungo, wakati kwenye benchi alikuwepo Gaudence Exavery
Mwaikimba.
Nasema sijui kwa sababu, Bunjak na wasaidizi wake ndiyo wana
siri ya timu yao, nani alikuwa katika hali gani, maana habari zilizopatikana
jana zinasema hata Bocco alicheza akiwa ana maumivu na kilichotokea jana
alitoneshwa tu hadi akatoka.
Bocco akimgeuza Ochieng |
Nachotaka kuzungumzia leo ni kwa nini mechi iliyotarajiwa
kuwa ngumu ikawa nyepesi mno- Azam kucheza bila mshambuliaji kuanzia dakika ya
20 ndiko kuliwapa ahueni Simba kwenye mchezo huo.
Wakati Bocco alipokuwa uwanjani, mabeki wa Simba walikuwa
hawaendi juu ili kumchunga hasa baada ya kuwafunga bao la kwanza na zaidi hata
viungo wakabaji, Jonas Mkude na Amri Kiemba nao walikuwa wanakwenda juu kwa
machale sana.
Hiyo iliwapa fursa kwa Azam kufanya mashambulizi zaidi langoni
mwa Simba na kukosa mabao kadhaa hata wakati timu hizo zikiwa 1-1.
Wakati Azam inaongoza 1-0, waliruhusu bao la kusawazisha kwa
makosa ya kawaida ya kimchezo na zaidi hata kipa Mwadini Ali jana hakuwa
vizuri, maana hakuwa na jitihada za ziada za kuiokoa timu yake na alikubali
kufungwa kiurahisi.
Lakini baada ya Simba kuona kosa lililofanywa na Azam
kufuatia kuumia kwa Bocco, wakawa huru na kushambulia kwa mapana marefu zaidi
zaidi.
Utaona hata Shomary Kapombe na Paschal Ochieng walikuwa wanapanda
pia, wabaki nyuma kumlinda nani na wapinzani hawana mshambuliaji?
Si kama Azam walizidiwa mchezo hapana, bali walidhibitiwa na
Simba kwa sababu hawakuwa na mchezaji hatari pale mbele. Kipre Tcheche ni mzuri
kweli, lakini ana aina ya mipira yake, muwekee kwenye njia akimbize, mwisho wa
siku atoe krosi, nani ataunganisha?
Krosi nzuri ziliendelea kutiwa kwenye lango la Simba na hata kona,
lakini nani angeunganisha? Nani angewatia misukosuko mabeki wa Simba?
Bunjak amekuwa akimtumia sana kiungo Abdulhalim Humud katika
mashambulizi yanayotokana na mipira ya kona, lakini jana alidhibitiwa na kwa
sababu Bocco hakuwapo, ilikuwa kazi rahisi mno.
Si dhambi Azam kufungwa na Simba, lakini inasikitisha mechi
iliyotarajiwa kuwa burudani zaidi, inakuwa ya kawaida sana, ukizingatia ligi
yenyewe ina mechi chache tu za kutazama.
Upande wa pili, kwa kuwa Azam watashiriki Kombe la Shirikisho
Afrika mwakani, mechi ngumu kama hizi, dhidi ya Simba na Yanga ndio kipimo kwao
cha kuujua ubora wa timu yao.
Sawa, Erasto Nyoni hakuwapo jana na badala yake akacheza
Samir Hajji Nuhu, sioni tofauti sana baina ya wachezaji hao, labda uzoefu tu,
lakini Mrisho Ngassa angeendelea kuwa hatari tu kwa Azam hata angekuwepo nani
Azam inahitaji kurudia orodha ya wachezaji iliyowasajili na kisha
ijiulize ina washambuliaji wangapi kikosini na wangapi wako tayari kucheza.
Mshambuliaji ni mshambuliaji tu, ana maarifa ya kupambana na
mabeki hasa kwenye mipira inayoelekezwa langoni kutoka pembeni mwa Uwanja. Mshambuliaji
anaongeza ladha ya timu kwa kiasi kikubwa sana.
Na ndiyo maana huyo ndiye mchezaji anayenunuliwa kwa bei
mbaya zaidi katika soko la wachezaji duniani.
Abdi Kassim ‘Babbi’ ana mwili mkubwa, lakini huyu bado ni
kiungo tu. Kama Azam haina mshambuliaji zaidi ya Bocco, lawama haziwezi kuwa za
Bunjak kwa sababu siye aliyesajili timu.
Lakini kwa Azam haitakuwa busara kutafuta mchawi kwa sasa,
nawaambia watumie mechi hizi dhidi ya Simba na Yanga kuiangalia timu yao
kuelekea mwakani katika Kombe la Shirikisho.
Hii ni timu ambayo ujio wake ulipokewa kama mwanzo wa mapinduzi
katika soka ya Tanzania, na kweli dalili tunaziona, ila itapendeza mapinduzi
yasiwe tu ya rasilimali, bali na soka pia uwanjani na matokeo mazuri.
Hivyo, wamalizie mechi za mzunguko wa kwanza huku wakikitathmini
kikosi chao na kufikiria namna ya kukiboresha katika usajili wa dirisha dogo
ambao utakuwa wa mwisho kuelekea michuano ya Afrika.