Hans Pope; Yanga acheni kudeka, chezeni soka |
Na Mahmoud Zubeiry
MWENYEKITI
wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe amewataka Yanga waache desturi
ya kutafuta mchawi nje ya timu yao mambo yanapowaendea mrama na badala yake ya
sasa waanze kuangalia matatizo yao ili kuyatatua.
Kauli hiyo
ya Kapteni wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), inakuja kufuatia
madai ya Yanga kwamba Simba wanatia ‘mkono’ kwenye mechi zao ndio maana
zinakuwa ngumu.
“Tatizo la
Yanga ni moja, wanapofanya vibaya, wanaanza kutafuta mchawi nje ya timu yao,
ona sasa wanasema Simba wanatia mkono mechi zao, kivipi? Kwa uchawi au kwa
nini?”alihoji Hans Poppe.
Hans Poppe
ambaye pia ni Mwenyekiti wa Friends Of Simba (F.O.S.) alisema kwamba kama Simba
wanakwenda kwa timu ambazo zinacheza Yanga na kuwapa motisha wacheze kwa nguvu,
haoni ubaya katika hilo, zaidi linasaidia maendeleo ya soka ya nchi hii.
“Lazima
wakabiliane na upinzani, ili wakishinda waonekane wana timu imara, wasitake
kushinda kwa urahisi rahisi, kwa hivyo ushauri wa bure tunaowapa Yanga, wao
wacheze mpira, waache kutafuta mchawi, kwa sababu kama wana uwezo watashinda tu,
hata timu ipewe motisha, watashinda kwa uwezo wao, ila kama hawana uwezo, ndio
hivi saasa wanaanza kutafuta mchawi,”alisema.
Yanga inadai
Simba SC ‘wanatia mkono’ kwenye mechi zao na ndio maana zinakuwa ngumu, ila
kuanzia sasa na wao wanaanza ‘fitina’.
Madai hayo
yanakuja, baada ya jana kuchapwa bao 1-0 na Kagera Sugar katika mchezo wake wa
sita wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, uliopigwa Uwanja wa Kaitaba, Bukoba.
“Simba
ilituma watu Bukoba watie mkono mechi yetu, sisi tuliwashitukia hao watu
baadaye sana, lakini tunashangaa kwa nini wanafanya hivi, wakati sisi
tulizungumza nao tukakubaliana haya mambo tuyaache, tucheze mpira, sasa wao
wanatuzunguka wanaendeleza mchezo mchafu,”alisema kiongozi Mjumbe mmoja wa
Kamati ya Mashindano ya Yanga, ambaye hakutaka kutajwa jina.
Mjumbe huyo
alisema kwamba wao walijua baada ya makubaliano na Simba kutofanyiana fitina,
waliamini mambo hayo hayatakuwapo, lakini baada ya kugundua wenzao wamewageuka
sasa na wao wanaanza ‘mchezo huo’.
“Na sisi
sasa tunaanza kuzicheza mechi zao, wakumbuke tu wao ndio walichokoza nyuki,
sasa subirini kuanzia mechi yao na Coastal, wakishinda wao wanaume, na pamoja
na kuzicheza mechi zao, tunajizatiti katika mechi zetu. Uzuri watu wote
wanaowatumia tumekwishawajua, ni wale wale waliokuja Morogoro, na wale wale
waliokuja Bukoba. Tumekwishawajua,”alisema Mjumbe huyo.
Bao pekee la
Themi Felix katika dakika ya 67, jana liliwapa Kagera Sugar ushindi wa 1-0
dhidi ya Yanga SC, kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba katika mchezo wa Ligi Kuu
ya Vodacom Tanzania Bara.
Felix
aliyeingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Mnigeria, Enyinna Darlington kwa
kumtungua bao hilo, kipa Mghana wa Yanga, Yaw Berko, ameendeleza rekodi yake
kuvifunga vigogo, Simba na Yanga katika Uwanja huo.
Hiyo inakuwa
mechi ya pili Yanga kufungwa ndani ya mechi sita walizocheza hadi sasa na mbili
wametoka sare- maana yake inabaki na pointi zake nane na kuzidi kujipunguzia
matumaini ya ubingwa msimu huu, ikiwa sasa inazidiwa pointi nane na vinara wa
ligi hiyo Simba SC.
Aidha, hii
ni mechi ya pili Yanga inacheza chini ya kocha wake mpya, Mholanzi Ernie
Blandts aliyerithi mikoba ya Mbelgiji, Tom Saintfiet na katika mechi hizo mbili
ameambulia pointi moja kutokana na sare dhidi ya Simba Jumatano.
Kwa ujumla
Yanga haijashinda hata mechi moja ya ugenini kati ya tatu ilizocheza hadi sasa,
ilitoka 0-0 na Prisons, ikafungwa 3-0 na Mtibwa na jana imechapwa 1-0 na Kagera
Sugar, wakati Alhamisi itacheza na Toto African mjini Mwanza.
Katika mechi
hiyo ya jana, Yanga ilipata pigo dakika ya 23 baada ya mshambuliaji wake mahiri
na tegemeo, Said Bahanuzi ‘Spider Man’ kuchanika nyama za paja dakika ya 23,
baada ya kugongana na beki Benjamin Effe wa Kagera Sugar na kushindwa kuendelea
na mchezo, nafasi yake ikichukuliwa na Jerry Tegete.
Tangu
ajiunge na Yanga akitokea Mtibwa Sugar msimu huu, leo Bahanuzi amecheza mechi
ya 13 kwa dakika hizo 23 na ameifungia timu hiyo jumla ya mabao 12, matatu kati
ya hayo kwa penalti.
Katika mechi
zilizochezwa juzi za ligi hiyo, Simba SC ilizidi kujiimarisha kileleni kufuatia
ushindi wa mabao 4-1 ilioupata kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam dhidi ya
JKT Oljoro ya Arusha, ambayo ilimaliza pungufu ya wachezaji wawili baada ya
kipa wake Shaibu Issa na mshambuliaji Meshack Nyambele kutolewa kwa kadi
nyekundu kipindi cha pili.
Katika mechi
hiyo iliyochezeshwa na refa Amon Paul wa Mara, aliyesaidiwa na Anold Bugabo wa
Singida na Charles Simon wa Dodoma, hadi mapumziko Simba walikuwa tayari mbele
kwa mabao 2-1, mabao yake yote yakitiwa kimiani na kiungo Amri Ramadhan Kiemba
katika dakika za 16 na 44, wakati la Oljoro lilifungwa na Paul Nonga dakika ya
29.
Kiemba
alifunga bao la kwanza akiunganisha krosi pasi ya Christopher Edward, wakati
bao la pili lilitokana na krosi ya Nassor Masoud ‘Chollo’, yote kutokana na
mashambulizi ya upande wa kulia.
Ilikuwa
rahisi kwa Kiemba kufunga mabao yote akiwa kwenye eneo la hatari, kutokana na
mabeki wa Oljoro kumuwekea ulinzi zaidi Felix Sunzu.
Nonga naye
alifunga bao lake baada ya kupewa pasi ndefu na kumpiga chenga kipa na Nahodha
wa Simba, Juma Kaseja upande wa kulia mwa Uwanja na kuutumbukiza mpira nyavuni
kiulaini.
Bao hilo
lilitokana na beki Paul Ngalema kupokonywa mpira wakati amepanda kusaidia
mashambulizi na Oljoro wakafanya shambulizi la haraka.
Kipindi cha
pili Simba walirudi vizuri zaidi uwanjani na kuuteka zaidi mchezo- jambo ambalo
liliwafanya Oljoro wawapunguze kasi kwa kuwachezea rafu. Hilo liliwagharimu
kupoteza wachezaji wao wawili kabla ya filimbi ya mwisho na kufungwa mabao
mawili zaidi.
Dakika ya 83
Mganda Emanuel Okwi aliifungia Simba bao la tatu na katika dakika ya tatu ya
muda wa nyongeza baada ya kutimu dakika 90 za mchezo, Okwi akiwa anaelekea
kufunga tena, alikwatuliwa na kipa wa Oljoro Shaibu Issa na refa akaamuru
penalti sambamba na kumtoa nje kwa kadi nyekundu ya moja kwa moja mlinda mlango
huyo.
Awali ya
hapo, Oljoro ilimpoteza mchezaji mwingine, Nyambele dakika ya 78, ambaye
alionyeshwa njano ya pili kwa rafu aliyomchezea Jonas Mkude. Nahodha Kaseja
alitaka kwenda kupiga, lakini akazuiwa na Felix Mumba Sunzu akaenda kufunga bao
la nne kwa mkwaju wa penalti.
Kwa ushindi
huo, Simba imefikisha pointi 16 baada ya kucheza mechi sita, hivyo kuendelea
kuongoza Ligi Kuu, ikifuatiwa na Azam yenye pointi 13, ingawa imecheza mechi
tano.
Katika mechi
nyingine za jana, Mgambo imepata ushindi wake wa kwanza baada ya kuichapa
Polisi Morogoro 1-0, wakati Toto African imeichapa JKT Ruvu 2-1 na Prisons
imelazimishwa sare ya bila kufungana na Mtibwa Sugar.