Na Ally Mohamed, Zanzibar
MSHAMBULIAJI wa Chipukizi, Faki Mwalim ndiye anayeongoza kwa
mabao kwa kupachika wavuni mabao matano mpaka sasa, katika Ligi Kuu ya Grand
Malt inayoendelea.
Timu zote mpaka sasa zimeshuka uwanjani mara tano, huku
Bandari ikiwa inaongoza ligi hiyo kwa kujikusanyia pointi 13, huku Falcon
ikiburuza mkia ikiwa na pointi moja tu.
Wakati Faki akiongoza kwa mabao hayo, anafuatiwa kwa karibu
na Ali Manzo Mnyovela wa Mtende mwenye mabao manne, huku waliofunga matatu
wakiwa ni Mohd Abdurahim wa Mtende na Amour Suleiman anayekipiga Malindi.
Wengine na timu wanazotoka kwenye mabano ni Mussa Omar
(Malindi), Mfaume Shaaban (Jamhuri) na Jaku Joma Jaku (Mafunzo), huku
aliyepachika mawili akiwa Haitham Khamis (Bandari).
Pamoja na Bandari kuongoza ligi hiyo kwa kujikusanyia pointi
hizo, inafuatiwa kwa karibu zaidi na Mtende yenye pointi 10.
Duma ndio yenye kadi nyingi za njano, ikiwa mpaka sasa
wachezaji wake wameonyeshwa kadi hizo mara 12, ikiwa pia na kadi moja nyekundu.
Mafunzo na Zimamoto kila moja ina kadi mbili nyekundu.
Ligi Kuu ya Grand Malt inatarajiwa kuendelea tena leo kwa
mchezo mmoja, wakati Mafunzo itakapoikaribisha Chuoni katika Uwanja wa Amaan,
wakati kesho Mtende itakuwa na kibarua kizito kwa KMKM katika uwanja huo.
Jumamosi Malindi itaivaa Chikupikizi ndani ya Uwanja wa
Amaan, huku kwenye Uwanja wa Gombani, Pemba kukiwa na pambano kati ya Duma na
Mundu na siku inayofuata Mafunzo ikiivaa Jamhuri ndani ya Amaan.
Ligi Kuu ya Zanzibar ambayo kwa sasa inajulikana kama Grand
Malt Premier League inadhaminiwa na kinywaji cha Grand Malt kisicho na kilevi.