Azam FC |
Na Mahmoud Zubeiry
USHINDI wa mabao 3-0 wa Coastal Union dhidi ya JKT Ruvu kwenye
Uwanja wa Chamazi, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam jana, umebadilisha kabisa
taswira ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, baada ya Wagosi hao wa Kaya
kupanda hadi nafasi ya tatu wakiiengua Azam.
Mapinduzi katika Ligi Kuu yalianza Jumamosi, baada ya Yanga kupanda
hadi nafasi ya pili kutokana na ushindi wao wa bao 1-0 dhidi ya JKT Oljoro,
Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha huku Azam FC ikifungwa na Simba SC
mabao 3-1 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kushuka nafasi ya tatu.
Lakini Coastal jana imeishusha Azam kwa nafasi moja zaidi, na
sasa mbio za ubingwa wa Ligi Kuu zinaonekana kuwa za farasi watatu, lakini Azam
si miongoni mwao, bali Simba, Yanga na Coastal.
Mwishoni mwa wiki ijayo, Yanga itacheza na Azam FC, mechi
ambayo itatengeneza taswira ya namna mzunguko wa kwanza utakavyomalizika.
Azam ikishinda inaweza kurudi nyuma ya Simba SC, lakini
tofauti na hapo watu watasubiri kuona kati ya watani hao wa jadi, nani
atamaliza mzunguko wa kwanza akiwa kileleni.
Kabla ya kucheza na Azam, Yanga itacheza Mgambo Shooting
Jumatano, wakati Azam itacheza na Coastal Union Chamazi.
Ligi Kuu sasa inazidi kunoga baada ya juzi Simba kuzinduka
kutoka kwenye wimbi la sare, baada ya kufanikiwa kuichapa Azam FC mabao 3-1
kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Ushindi huo, unaifanya Simba izidi kujitanua kileleni mwa
ligi hiyo kwa kufikisha pointi 22, baada ya kucheza mechi 10, wakati Azam FC
inapromoka hadi nafasi ya nne kwa pointi zake 18, baada ya kucheza mechi tisa,
ikiipisha Coastal yenye pointi 19 katika nafasi ya tatu na Yanga sasa ni ya
pili kwa pointi zake 20.
Mechi nyingine za ligi hiyo juzi, African Lyon ilitoka sare
ya 1-1 Kagera Sugar Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam na Ruvu Shooting ikaifunga
2-1 Polisi Morogoro Uwanja wa Mabatini, Mlandizi.
Mechi kati ya Mgambo JKT na Prisons iliyokuwa ichezawe juzi
Uwanja wa Mkwakwani, Tanga imeahirshwa kutokana na wachezaji wa Prisons kupata
ajali wakiwa njiani kuelekea Tanga.
JKT Ruvu jana ilifungwa 3-0 na Coastal Union Uwanja wa Chamazi,
Dar es Salaam na Toto Africans ilitoka sare ya 1-1 na Mtibwa Sugar Uwanja wa
CCM Kirumba, Mwanza.