Coastal Union ya 2012 |
Na Princess Asia
KUELEKEA mechi ya kesho dhidi ya Coastal
Union, Uwanja wa Mkwakwani, Tanga Simba SC inawahofia zaidi wachezaji wake wa zamani
ambao kwa sasa wanachezea kwa wapinzani wa hao wa kesho.
Gumzo ndani ya Simba kuelekea
mchezo huo ni namna ambavyo wachezaji wao waliowatema na sasa wanachezea
Coastal watakavyojituma katika mechi hiyo ili kuonyesha wao bado wachezaji
wazuri.
Wachezaji wa zamani wa Simba kwenye
kikosi cha Cosatal ni mabeki Said Swedi ambaye ni Nahodha wa timu, Juma Jabu, kiungo
Jerry Santo na washambuliaji Nsa Job na Sali Aziz Gilla.
Wachezaji wote hao huwa wanaanza
kwenye kikosi cha kwanza cha Cosatal na kesho pia, kuna uwezekano Swedi ‘Panucci’
akaanza beki ya kulia na JJ akacheza kushoto, wakati kwenye kiungo Mkenya, Santo
ataichezesha timu.
Kuna uwezekano mkubwa sana Salim
Aziz Gilla akatokea benchi, lakini ‘piga ua’, mkali wa mabao, Nsa Job lazima
ataanza kwenye mechi hiyo kujaribu kufanya kile alichokifanya msimu uliopita
akiwa Villa Squad, kutikisa nyavu za Simba kwa bao muhimu.
Lakini pia, kikosi cha mabingwa hao
wa Ligi Kuu 1988, kina wachezaji wengine wa kutisha kama kiungo Razack Khalfan
aliyewahi kucheza Yanga na mshambuliaji wa timu ya taifa ya vijana chini ya
umri wa miaka 20, Atupele Green, ambaye huenda akaanza na Nsa kesho pale mbele.
Yupo beki Mganda Philip Kaira na kiungo wa kimataifa wa Zanzibar, Suleiman Kassim 'Selembe'- wote wanatisha na kesho bila shaka wataipa mtihani Simba SC Mkwakwani.
Simba inaendelea vizuri kwa
maandalizi yake ya mchezo huo wa kesho dhidi ya wenyeji Coastal Union mjini
Tanga na wachezaji wote 22 waliokwenda huko wana morali ya kutosha ya ushindi.
Vigogo wa Friends Of Simba (F.O.S)
wakiongozwa na Mwenyekiti wao, Zacharia Hans Poppe wamekodi ndege kwenda Tanga
kuwaongezea morali washinde mechi ya kesho, ambayo inatarajiwa kuwa ngumu
kutokana wenyeji kupania kuwa timu ya kwanza kuifunga Simba msimu huu.
Ikumbukwe Simba imetoa sare moja ya
kufungana 1-1 na Yanga, Oktoba 3, mwaka huu katika mechi zake sita ilizocheza
sasa na nyingine zote tano imeshinda, jambo ambalo linawafanya waendelee kuwa
kileleni mwa Ligi Kuu.
Simba, ambayo kwenye mechi hiyo
itawakosa nyota wake saba, Emanuel Okwi ambaye amekwenda kujiunga na timu yake
ya taifa, Uganda, Ramadhani Chombo ‘Redondo’, Mrisho Khalfan Ngassa
wanaosumbuliwa na Malaria, Haruna Shamte, Kiggi Makassy Kiggi, Hamadi Waziri na
Komabil Keita ambao ni majeruhi ipo Tanga tangu juzi.
Wachezaji 22 walio na timu Tanga ni
makipa Juma Kaseja, Wilbert Mweta, mabeki Nassor Masoud ‘Chollo’, Amir Maftah, Juma
Nyoso, Paschal Ochieng, Shomary Kapombe, Hassan Khatib, Paulo Ngalema, Komabil
Keita, viungo Mwinyi Kazimoto, Jonas Mkude, Amri Kiemba, Salim Kinje, Ramadhani
Singano, Uhuru Suleiman, Haruna Moshi ‘Boban’ na washambuliaji Felix Sunzu,
Edward Christopher, Haroun Chanongo, Daniel Akuffo na Abdallah Juma.
Katika kujiandaa na mechi ya Tanga,
Simba Jumanne ilicheza mechi ya kujipima nguvu na kuifunga Azam FC mabao 3-2
katika mchezo wa kirafiki uliofanyika asubuhi kwenye Uwanja wa Chamazi, maarufu
kama Azam Complex, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Mabao ya Simba siku hiyo yalifungwa
Ramadhani Singano ‘Messi’, Uhuru Suleiman ‘Robinho’ na Daniel Akuffo, wakati ya
Azam yalifungwa na Jamil Mchauru na Khamis Mcha.
Hiyo ilikuwa mechi ya nne Azam
inafungwa na Simba msimu huu katika mechi tano walizokutana hadi sasa, baada ya
awali kufungwa kwa penalti kwenye fainali ya Kombe la Urafiki, kufuatia sare ya
2-2, kufungwa 2-1 kwenye Nusu Fainali ya BancABC Sup8R na 3-2 kwenye mechi ya
Ngao ya Jamii, wakati wao walishinda 3-1 dhidi ya Wekundu hao wa Msimbazi,
katika Robo Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame.
Azam na Simba zitakutana tena
katika mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, mzunguko wa kwanza, Oktoba
27, mwaka huu, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Simba ndio inaongoza Ligi Kuu, hadi
sasa ikiwa imeshinda mechi tano kati ya sita ilizocheza na moja tu imetoka
sare, hivyo kujikusanyia pointi 16, wakati Azam inashika nafasi ya pili
ikizidiwa pointi tatu, ingawa pia iko nyuma kwa mchezo mmoja.