Brandts |
Na Prince Akbar, Mwanza
BAADA ya ushindi wa mabao 3-1 jana dhidi ya wenyeji Toto
African katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Uwanja wa CCM
Kirumba mjini Mwanza, Yanga wanarejea leo Dar es Salaam kwa basi leo kujiandaa
na mchezo ujao, dhidi ya Ruvu Shooting Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Oktoba
20, mwaka huu.
Kocha Mholanzi, Ernie Brandts atakuwa na muda wa kutosha wa
kurekebisha makosa katika kikosi chake kabla ya kuingia kwenye mchezo wa nane
wa Ligi Kuu na wa nne tangu aanze kazi, akirithi mikoba ya Mbelgiji, Tom
Saintfiet.
Katika siku za karibuni, mapungufu ya wazi yaliyojitokeza
kwenye kikosi cha Yanga ni kucheza bila uelewano wa kutosha, umakini haba na
pia wachezaji wanaonekana hawana stamina ya kutosha, mambo ambayo yameigharimu
timu hiyo kupoteza mechi mbili katika saba walizocheza, mbili wakitoa sare na kushinda
tatu.
Yanga SC jana ilizinduka kutoka kwenye kipigo cha 1-0
walichopewa na Kagera Sugar mjini Bukoba Jumatatu na kushinda mabao 3-1 katika
mfululizo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, dhidi ya wenyeji Toto African,
kwenye Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza.
Matokeo hayo, yaliifanya Yanga itimize pointi 11, katika
mechi saba ilizocheza hadi sasa, ikiwa imefungwa mbili, sare mbili na kushinda
tatu, inazidiwa pointi tano na wapinzani wake wa jadi, Simba SC wanaoongoza
ligi hiyo kwa pointi zao 16, wakifuatiwa na Azam wenye pointi 13.
Hadi mapumziko, Yanga walikuwa tayari mbele kwa mabao 2-0, yaliyopachikwa
kimiani na mshambuliaji wa kimataifa wa Burundi, Didier Kavumbangu na beki wa
kimataifa wa Rwanda, mwenye asili ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC),
Mbuyu Twite.
Kavumbangu alifunga bao la kwanza dakika ya pili, baada ya
kuuwahi mpira uliotemwa na kipa Erick Ngwengwe kufuatia kona iliyochongwa na
Haruna Niyonzima, hilo likiwa bao lake la tano ndani ya mechi 11 tangu ajiunge
na Yanga msimu huu akitokea Atletico ya kwao, Burundi.
Baada ya bao hilo, Yanga waliendelea kulisakama lango la Toto
na dakika ya 21, Mbuyu Twite akaunganisha kona ya chini chini iliyochongwa na
Niyonzima.
Toto ilipoteza nafasi nzuri ya kufunga dakika ya 42, baada ya
kupata penalti, kufuatia beki mmoja wa Yanga kuunawa mpira kwenye eneo la
hatari, baada ya Wana Kishamapanda kufanya shambulizi kali la kushitukiza,
lakini kiungo Emanuel Swita akapiga nje.
Swita alipiga penalti nzuri tu ya chini pembeni kabisa,
lakini vipimo vyake vikazidi kidogo, mpira ukatoka nje, ingawa Berko aliifuata
vizuri pembeni kabisa kulia kwake na angeweza kuokoa.
Kipindi cha pili Toto waliingia kwa kasi zaidi na kuanza
kulishambulia lango la Yanga mfululizo, wakitawala zaidi sehemu ya kiungo.
Katika dakika ya 54 mshambuliaji Mussa Said aliifungia Toto
bao safi, baada ya kipa Yaw Berko kutoka langoni.
Baada ya bao hilo, Toto walizidi kutawala mchezo na kukosa
mabao mawili ya wazi- hapo ndipo kocha Mholanzi, Ernie Brandts akawatoa viungo
Frank Domayo na Athumani Idii ‘Chuji’ na kuwaingiza Shamte Ally na David
Luhende.
Walipoingia Shamte na Luhende wote walienda kushambulia
pembeni na Haruna Niyonzima na Nurdin Bakari wakarudi katikati.
Mabadiliko hayo yaliisaidia Yanga kupata bao la tatu dakika
ya 68, lililofungwa kitaalamu na mshambuliaji Jerry Tegete ambaye alimpiga
chenga kipa Ngwengwe baada ya kupokea pasi ya Oscar Joshua.
Baada ya bao hilo, Kocha wa Toto, Johh Tegete naye alifanya
mabadiliko akiwatoa Mussa Said na Evarist Maganga na kuwaingiza Heri Mohamed na
Heri Kyaruzi. Hata hivyo, pamoja na mabadiliko hayo, Yanga waliendelea kutawala
mchezo hadi filimbi ya mwisho.
Kwa ushindi huu, Yanga imelipa kisasi cha mara ya mwisho timu
hizo, zilipokutana kwenye Uwanja huo, Jumapili ya Aprili 15, mwaka huu, Toto
walipoibuka na ushindi wa mabao 3-2.
Katika mchezo huo, kikosi cha Yanga kilikuwa; Yaw Berko, Juma
Abdul, Oscar Joshua, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Mbuyu Twite, Athumani Iddi
‘Chuji’/Shamte Ally, Frank Domayo/David Luhende, Haruna Niyonzima, Jerry Tegete,
Didier Kavumbangu na Nurdin Bakari.
Toto; Erick Ngwengwe, Kulwa Greyson, Eric Mulilo, Evarist
Maganga/Heri Kyaruzi, Peter Mabula, Hamisi Msafiri, Emanuel Swita, Haroun
Athumani, Mohamed Hussein, Suleiman Kibuta na Mussa Said/Heri Mohamed.