Kiiza |
Na Mahmoud Zubeiry
MWENYEKITI wa Kamati ya Mashindano ya klabu ya Yanga,
Abdallah Ahmed Bin Kleb jana ‘aliwawakia’ wachezaji wa mbele wa timu hiyo kwa
uchoyo wa pasi na kukemea tabia inayoonekana kuanza kujitokeza, wachezaji wa
timu hiyo kutopendana.
Bin Kleb aliingia ‘kwa hasira’ chumba cha kubadilishia nguo
cha Yanga na kuanza kufoka juu ya tabia hiyo, akisema timu inatengeneza nafasi
nyingi, lakini kwa uchoyo wa baadhi ya wachezaji kutoa pasi kwa wenzao walio
kwenye nafasi nzuri zaidi, inaambulia mabao machache.
Bosi huyo alifanya hivyo baada ya mechi dhidi ya Polisi
Morogoro kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, ambayo Yanga ilishinda 3-0.
Lakini pia Bin Kleb alimuuliza kocha Mkuu, Mholanzi Ernie Brandts
kwa nini timu haichezi vizuri pamoja na kushinda. Brandts alitumia hekima
kukwepa kujibu swali mbele ya wachezaji, lakini baadaye alimvuta pembeni Bin
Kleb wakazungumza.
Tayari kuna dalili za mgawanyiko ndani ya Yanga baina ya
wachezaji na hilo lilijidhihirisha wakati Hamisi Kiiza alipofunga bao lake
lililokuwa la tatu katika ushindi wa 3-0, hakwenda kushangilia na wachezaji wenzake,
bali alimkimbilia kipa wa akiba, Mghana Yawe Berko kushangilia naye jana.
Ingawa hajawahi kulalamika, lakini ukiifuatailia Yanga tangu
baada ya michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame,
Kiiza ndiye ambaye mara nyingi amekuwa hapewi pasi na wenzake anapokuwa kwenye
nafasi nzuri, ingawa yeye amekuwa anawapa tu wenzake pasi za mabao.
Pamoja na hayo, hali hiyo inaonekana kidogo kuathiri uchezaji
wa Kiiza, anayeonekana kuwa mnyonge na asiye na raha uwanjani na haikushangaza
alipotolewa nje kipindi cha kwanza kwenye mechi dhidi ya Simba, Oktoba 3, mwaka
huu.
Lakini Kiiza amekuwa akicheza kwa kiwango cha juu mno katika
timu yake ya taifa, Uganda, The Cranes pamoja na ‘kusuasua’ Yanga.