Benjamin Effe akumdhibiti Mrisho Ngassa |
Na Mahmoud Zubeiry
BEKI Mnigeria wa Kagera Sugar, Benjamin Effe Ofuyah ameanza
kuvitoa udenda vigogo vya soka Tanzania, Simba na Yanga kutokana na soka yake
maridadi anayoonyesha katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Beki huyo wa kati aliwavutia Yanga walipokwenda Bukoba
kucheza na Kagera Sugar Oktoba 8, katika mechi ambayo wenyeji walishinda 1-0,
bao pekee la mkongwe Themi Felix kwenye Uwanja wa Kaitaba.
Effe aliwavutia pia Simba katika mchezo wa juzi Uwanja wa Taifa,
Dar es Salaam wakati Kagera ikilazimisha sare ya kufungana mabao 2-2 na wenyeji
wao.
Effe ambaye anacheza kama sentahafu, akiwa pacha wa Amandus
Nesta katika mechi na Simba alionyesha uwezo mkubwa wa kulinda na kusaidia mashambulizi.
Ana uwezo mkubwa wa kumiliki mpira, kasi kuruka hewani
kuicheza mipira kwa kichwa- nguvu za kupambana na washambuliaji na zaidi ni
mtulivu, asiye na papara, mwenye maamuzi ya haraka.
Mara kadhaa alishinda mipira dhidi ya washambuliaji hatari wa
Simba, akina Mzambia Felix Mumba Sunzu Jr., Mganda Emmanuel Arnold Okwi na mzalendo
Mrisho Khalfan Ngassa.
Beki huyo amesajiliwa na Kagera Sugar kwa pamoja na mwenzake,
mshambuliaji Wilfred Emmeh kutoka klabu ya Abuja FC ya kwao Nigeria. Kwa ujumla,
katika kikosi cha Kagera kuna Wanigeria watatu, mwingine ni Enyinna Darlington
ambaye amesajiliwa kutoka Toto African ya Mwanza, ambayo nayo ilimtoa Abuja FC
ya Nigeria.
Kagera Sugar ni moja yenye timu zenye kusifika kwa kuvumbua
vipaji, ambavyo baadaye vinanunuliwa kwa bei chafu na vigogo wa soka nchini,
Simba, Yanga na hata Azam FC.
Mrisho Ngassa, Amri Kiemba wa Simba, Said Mourad wa Azam FC,
Godfrey Taita na David Luhende wa Yanga, wote hawa wametokea Kagera Sugar.
Aidha, Kagera pia imekuwa ikiwarudisha wachezaji ambao
wameonekana hawafai timu nyingine na kuwa na thamani tena, mfano Gaudence Exavery
Mwaikimba aliyetupiwa virago Yanga akaenda kufufua makali yake huko, hatimaye
kusajiliwa na Azam FC msimu uliopita.
Salum Kanoni Kupela aliyetupiwa virago Simba SC hivi sasa anang’ara
Kagera Sugar na ndiye aliyeifungia timu hiyo bao la kusawazisha kwa penalti katika
mechi dhidi ya Wekundu wa Msimbazi, siku ambayo alionekana kumdhibiti vizuri Okwi.