Bahanuzi |
Na Mahmoud Zubeiry
BEKI Kevin
Yondan na mshambuliaji Said Bahanuzi wataendelea kuwa nje ya Uwanja mwishoni
mwa wiki, wakati timu yao, Yanga SC itakapokuwa ikiwania pointi tatu katika
mfululizo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, kutokana na hali zao
kutoimarika.
Wawili hao
ambao ni majeruhi, wapo kwenye programu ya mazoezi mepesi na hadi jana hakuna
mmoja kati yao aliyekuwa tayari kuanza programu kamili ya mazoezi ya kocha
Mholanzi, Ernie Brandts.
Maana yake,
Mbuyu Twite ataendelea kucheza pamoja na Nadir Haroub ‘Cannavaro’ katika beki
ya kati, wakati Jerry Tegete ataendelea kucheza na Didier Kavumbangu katika
safu ya ushambuliaji.
‘Dogo’ Simon
Msuva amemaliza adhabu ya kadi nyekundu aliyopewa Oktoba 3, mwaka huu katika
mechi dhidi ya Simba na Hamisi Kiiza amerejea kutoka Uganda, alipokwenda
kuichezea timu yake ya taifa, The Cranes katika mchezo wa marudiano wa kuwania
tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwakani nchini Afrika
Kusini.
Uganda ilitolewa na Zambia kwa mikwaju ya penalti baada ya
sare ya jumla ya 1-1, Zambia wakianza kushinda nyumbani 1-0 na Uganda
wakashinda kwao 1-0 pia mwishoni mwa wiki, hivyo mchezo kuhamia kwenye mikwaju
ya penalti, ambako timu ya Kiiza ilitolewa.
Yanga imeweka kambi katika hoteli ya Uplands, Changanyikeni, Dar
es Salaam huku ikiendelea kufanya mazoezi kwenye Uwanja wa shule ya sekondari
ya Loyola, Mabibo, Dar es Salaam.
Beki Kevin Yondan aliyeumizwa na kiungo wa Simba, Haruna
Moshi ‘Boban’ katika mechi baina ya wapinzani hao wa jadi, Oktoba 3, mwaka huu,
wakati Bahanuzi ‘Spider
Man’ alichanika nyama za paja la mguu wa kulia katika mechi ya Ligi Kuu ya
Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba Oktoba
8, mwaka huu.
Bahanuzi
aliumia dakika ya 23, baada ya kugongana na beki Benjamin Effe wa Kagera Sugar
na kushindwa kuendelea na mchezo, nafasi yake ikichukuliwa na Jerry Tegete
katika mechi ambayo Yanga ililala 1-0, beo pekee la Themi Felix.
Bahanuzi
ndiye tegemeo la mabao la Yanga kwa sasa, kwani tangu ajiunge na timu hiyo
akitokea Mtibwa Sugar msimu huu, ameifungia mabao 12 katika mechi 13, ikiwemo
ile dhidi ya Kagera aliyocheza kwa dakika 23 kabla ya kuumia na kutoka.
Yanga kwa
sasa inashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu kwa pointi zake 11,
baada ya kucheza saba, kushinda tatu, sare mbili na kufungwa mbili.
Simba
iliyocheza mechi nane, inaongoza ligi hiyo kwa pointi zake 18, ikifuatiwa na
Azam FC yenye pointi 17, iliyocheza mechi saba.