Azim Dewji |
Na Prince Akbar
WAKATI klabu za Yanga na African
Lyon zikiendelea kusuguana na mdhamini wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, kampuni ya
simu ya mkononi ya Vodacom, klabu za soka nchini zimeaswa kuanza kujitambua ili
ziweze kunufaika kwa mambo mengi zaidi, badala ya kutumia muda mrefu kulumbana
kwa mambo madogo, akitolea mfano wa nembo ya Vodacom katika
jezi za klabu.
Ushauri huo umetolewa na mfadhili
wa zamani wa Simba, mfanyabiashara Azim Dewji aliyesema kuwa, kama klabu za
Tanzania zingekuwa zinajitambua, kamwe zisingepoteza muda kwa malumbano ya
nembo, bali maslahi.
Akizungumza na BIN ZUBEIRY leo, alisema
klabu kubwa kama Simba na Yanga, zinapaswa kujenga hoja nzito kwa wadhamini,
ilin ziweze kunufaika zaidi kwa kuwa zina thamani kubwa kutokana na ukongwe
wake na utajiri wa wafuasi kote ndani na nje ya Tanzania.
“Sawa wana haki, lakini klabu zetu
ifike mahali zijitambue.
Wavuke hapo, mfano Simba na Yanga
si zijenge hoja za kupata fedha zaidi kwa wadhamini kwamba ili zivae jezi na
nembo, zilipwe vizuri kulingana na hadhi halisi ya klabu hizi.
“Haiingii akilini kuona zimeshindwa
kujenga ushawishi hata baada ya kuwekwa kundi moja na timu ambazo hazina
wanachama wala ofisi, lakini kwa mujibu wa mkataba zote zinalipwa sh milioni 7
kwa mwezi.
“Jamani, hivi Yanga yenye utitiri
wa wanachama na wafuasi, utajiri wa majengo mfano jingo lake lina thamani ya
bilioni 2, inalipwaje sawa na African Lyon ambayo haina wanachama wala ofisi? “Si
kama naidharau Lyon, la hasha, bali ndio uhalisia kwa sababu kama
ni kunufaika, Vodacom itanufaika
zaidi kwa Yanga kutokana na wafuasi wake wengi kuliko Lyon, kwanini wasitumie
mwanya huo kujenga hoja?”
alihoji Dewji na kuongeza kuwa,
hadhi ya klabu za Simba na Yanga ni angalau kila moja iambulie sh milioni 250
kwa mwaka, na jezi za hadhi ya juu kulingana na hadhi ya klabu zenyewe.
Aidha, alisema udhamini mnono wa
Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) ni uthibitisho tosha kuwa thamani ya Simba na
Yanga. TBL kupitia bia ya Kilimanjaro, inazidhamini Simba na Yanga kila moja
kwa wastani wa sh bilioni 1.5 kwa mwaka, udhamini ukigusa mishahara ya
wachezaji na benchi la ufundi, mabasi, vifaa vya michezo, gharama za mikutano
ya
kila mwaka na kadhalika.
“Una sasa, TBL si wadhamini wakuu
wa soka ya nchi hii, lakini klabu hizi zinanufaika, kama ukweli ndio huo kwa
nini wasimbane mdhamini wa ligi ili wanufaike zaidi na badala yake wanabaki na
malumbano ya nembo pekee? Ni wakati wa klabu zetu kubadilika kwa sababu kote
ulimwenguni, soka ni biashara kubwa mno,” alisema.
Kauli ya Dewji imekuja huku klabu
za Yanga na Lyon zikiwa katika mgogoro juu ya kutovaa jezi zenye nembo ya
Vodacom, Yanga ikisema haiko tayari kuvaa jezi zenye nembo nyekundu ya mdhamini
huku Lyon ikitaka iruhusiwe kuvaa jezi za mdhamini wake binafsi, kampuni nyingine
ya simu za mkononi ya Zantel.
Kutokana na mvutano huo, klabu hizo
zimejiingiza katika hatari ya kuadhibiwa, kwani Shirikisho la Soka nchini (TFF)
limetishia kuchukua hatua dhidi ya klabu zinazokwenda kinyume na matakwa ya
mkataba wa udhamini wa Ligi Kuu ambao hata hivyo klabu zinalalamikia kuwa hauko
wazi.