Azim Dewji |
Na Princess Asia
MFANYABIASHARA maarufu nchini na
mfadhili wa zamani wa Simba, Azim Dewji amesema baadhi ya wanahabari nchini
wanachangia matokeo mabaya ya Yanga katika michuano ya mwaka huu ya Ligi Kuu ya
Tanzania Bara.
Amesema wamekuwa wakiingiza zaidi
ushabiki, badala ya kuisaidia timu hivyo kuwafanya wachezaji kulewa sifa mapema
hata pasipostahili, hali inayozifanya klabu nyingine kucheza kwa kukamia kwa
hofu ya kubebesha kapu la magoli.
Dewji aliyasema hayo jana, alipokuwa
anazungumzia kupepesuka kwa Yanga, licha ya kufanya usajili tishio msimu huu.
Katika mechi sita za ligi msimu
huu, Yanga imeshapoteza mechi mbili, imetoka sare mara mbili na kushinda mara
mbili, hivyo kuifanya kufikisha pointi nane ambazo ni nusu ya pointi
zilizokusanywa na watani wao Simba wanaoongoza ligi baada ya kukusanya pointi
16 kutokana na mechi sita pia.
Akiichambua Yanga, alisema
imesajili vizuri, lakini waandishi wa habari wamechangia kuwavimbisha vichwa
wachezaji kwa kuupamba mno usajili wao, ilhali ni wachezaji wa kawaida.
“Kama mwanamichezo, sioni tatizo
kwa timu wala benchi la ufundi, nadhani waandishi wanaoishabikia Yanga
wanaimaliza timu yao bila kujijua. Wanaikuza mno kuanzia kipindi cha
usajili..kila anayesajiliwa anapambwa kupita maelezo.
“Matokeo yao wanavimba vichwa,
mashabiki wanajazwa matumaini makubwa, na timu pinzani, hata kama ni ndogo
zinakamia zikihofia kugeuzwa kapu la magoli na hii timu inayotajwa kuwa tishio
kabisa, wakati ukweli sivyo…” anasema.
Aliongeza kusema: “Nashukuru Simba
tulifungwa na Azam 3-1 katika Kagame. Ile ilitushitua, tukatuliza akili na
ndiyo maana unaona timu imesukwa upya na iko imara. Tungetwaa ubingwa hakika
Simba hii ingekuwa nyeupe, tungelewa sifa tu. Soka haiko hivyo, kwa hiyo waandishi
wasiegemee ushabiki pekee, wazisaidie timu zao pia.”
Dewji alisisitiza kuwa, pamoja na
nia ya kufanya biashara, vyombo vya habari vinapaswa kusimama katika ukweli,
badala ya kusifia kila kinachoonekana, huku mambo yasiyofaa yakifunikwa kwa
hofu ya kuwakera wahusika.
“Haya yanayotokea katika soka, hasa
Simba na Yanga hayana tofauti na jinsi waandishi wanavyojaribu kukuza kila kitu
cha Chadema, kiasi cha kujiona wamefika juu mno kisiasa, sikatai ni chama
chenye wafuasi wengi, lakini washauriwe jinsi ya kujipanga hatua kwa hatua
kuliko
kuwajaza matumaini na matokeo yake
utakuta kila kinachofanyika, wanajiona wanaonewa…waandishi wawe washauri wazuri
jamani,” alisema Dewji.