Kikosi cha Azam |
Na Mahmoud Zubeiry
AZAM FC imerejea Dar es Salaam jana majira ya saa 1:00
ikitokea Mbeya, ambako juzi ililazimishwa sare ya bila kufungana na Prisons
kwenye Uwanja wa Sokoine, katika mfululizo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania
Bara.
Azam sasa wanaingia kambini kujiandaa na mchezo wao ujao,
Jumatano dhidi ya Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Chamazi, maarufu kama Azam Complex,
Dar es Salaam.
Pamoja na sare hiyo, Azam wamelalamikia uchezeshaji mbaya wa
marefa wa mechi hiyo, kwamba uliwapokonya ushindi.
Azam FC wanadai refa alikataa mabao yao mawili yaliyofungwa na
Abdi Kassim ‘Babbi’ na penalti ya wazi, baada ya kiungo Salum Abubakar ‘Sure
Boy Jr.’ kuangushwa kwenye eneo la hatari
Wanadai bao la kwanza, refa alilolikataa ulikuwa ni mkwaju wa
mbali wa Abdi Kassim ambao ulitinga nyavuni, kabla ya kurudi uwanjani na refa
licha ya kuona kuwa lilikuwa ni bao halali, bado akaamua kukataa
Wanadai baadaye, Sure Boy alifanyiwa madhambi kwenye eneo la hatari
na kwa mshangao wa wengi, wakiwemo viongozi na wachezaji wa Prisons ambao
walishashika vichwa, refa akapeta na mpira kuendelea
Zikiwa zimesalia dakika chache kabla ya mpira kumalizika,
Azam FC wanadai walipata adhabu ndogo na Abdi Kassim aliupiga mpira ule na
kutinga nyavuni, lakini kwa mara nyingine tena refa akakataa bao kwa madai kuwa
kabla ya kufunga, Babbi alikuwa ameotea.
Baada ya ‘kufanyiwa dhuluma’ hiyo, Azam wanaendelea kushika
nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu, wakiwa wana pointi 17, baada ya
kucheza mechi sana, wakati mabingwa watetezi, Simba SC wapo kileleni kwa pointi
zao 18 na wamecheza mechi nane.