Azam FC |
Na Mahmoud Zubeiry
AZAM FC inatarajiwa kuondoka leo
mchana kwenda Morogoro, tayari kwa mchezo wao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania
Bara dhidi ya wenyeji Polisi, kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.
Azam kwanza watafanya mazoezi
kwenye Uwanja wa Chamazi asubuhi ya leo, na baada ya hapo watapanda basi lao,
lenye kila kitu ndani- TV, friji, choo, mziki wa maana na siti za kulala kwa
safari ya takriban saa mbili kwenda Mji Kasoro Bahari.
Azam imepania kushinda mechi hiyo
Jumamosi ili kuiondoa Simba kileleni na kuzidi kuweka hai matumaini ya kutwaa
ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu.
Katika kujiandaa na mechi ya Morogoro,
Azam juzi ilicheza mechi ya kujipima nguvu na kufungwa na Simba SC mabao 3-2
katika mchezo wa kirafiki uliofanyika asubuhi kwenye Uwanja wa Chamazi, maarufu
kama Azam Complex, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Mabao ya Simba juzi yalifungwa
Ramadhani Singano ‘Messi’, Uhuru Suleiman ‘Robinho’ na Daniel Akuffo, wakati ya
Azam yalifungwa na Jamil Mchauru na Khamis Mcha.
Hiyo ilikuwa mechi ya nne Azam
inafungwa na Simba msimu huu katika mechi tano walizokutana hadi sasa, baada ya
awali kufungwa kwa penalti kwenye fainali ya Kombe la Urafiki, kufuatia sare ya
2-2, kufungwa 2-1 kwenye Nusu Fainali ya BancABC Sup8R na 3-2 kwenye mechi ya
Ngao ya Jamii, wakati wao walishinda 3-1 dhidi ya Wekundu hao wa Msimbazi,
katika Robo Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame.
Azam na Simba zitakutana tena
katika mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, mzunguko wa kwanza, Oktoba
27, mwaka huu, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Simba ndio inaongoza Ligi Kuu, hadi
sasa ikiwa imeshinda mechi tano kati ya sita ilizocheza na moja tu imetoka
sare, hivyo kujikusanyia pointi 16, wakati Azam inashika nafasi ya pili
ikizidiwa pointi tatu, ingawa pia iko nyuma kwa mchezo mmoja.