Azam FC |
Na Mahmoud Zubeiry
AZAM FC inaweza kupanda kileleni mwa Ligi Kuu ya Vodacom
Tanzania Bara Jumatano iwapo itaifunga Ruvu Shooting katika mfululizo wa ligi
hiyo, kwani itafikisha pointi 20 baada ya kucheza mechi nane na bado itakuwa
inazidiwa mchezo mmoja na vinara wa sasa wa ligi hiyo, Simba SC.
Haya yatakuwa mabadiliko ya kwanza kileleni mwa ligi hiyo
tangu kuanza kwake, Septemba 15 mwaka huu, kwani ni Simba imekuwa ikiongoza
muda wote. Matumaini ya Azam kupaa kileleni Jumatano, yanafuatia jana Simba SC
kulazimishwa sare ya 0-0 na wenyeji Mgambo JKT kwenye Uwanja wa Mkwakwani,
Tanga.
Simba sasa ina pointi 19, baada ya kucheza mechi tisa na Azam
ina pointi 17, baada ya kucheza mechi saba, wakati Yanga iliyocheza mechi nane,
ina pointi 14 katika nafasi ya tatu.
Simba ilianza vema Ligi Kuu, ikishinda mechi tano mfululizo,
lakini tangu itoe sare ya 1-1 na Yanga Oktoba 3, mwaka huu, ilishinda mechi
moja tu kati ya nne zilizofuata, Oktoba 7, mwaka 2012 ilipoifunga 4-1 JKT
Oljoro Uwanja wa Taifa.
Mechi tatu zilizofuata Simba imetoa sare zote, bila kufungana
na Mgambo na Coastal Union mjini Tanga na 2-2 na Kagera Sugar, Uwanja wa
Taifa.
Kocha Bunjak kushoto akijadiliana jambo na Meneja wa Azam, Patrick Kahamele wakati wakiifuatilia Ruvu Shooting ilipokuwa ikicheza na Yanga Jumamosi Uwanja wa Taifa |
Hadi sasa, Azam na Simba ndio timu pekee ambazo hazijafungwa
katika Ligi Kuu na hii inaashiria kwamba bado hizo ndizo timu bora katika ligi
hiyo, zikiendeleza upinzani wao wa tangu msimu uliopita.
Msimu uliopita, Simba ilitwaa ubingwa na Azam ikawa ya pili,
wakati Yanga iliambulia nafasi ya tatu na hadi sasa katika msimamo wa Ligi Kuu,
mpangilio uko hivyo ingawa ni matarajio ya wengi keshokutwa mambo yatabadilika.
Lakini pia mbele ya Ruvu Shooting iliyoonyesha upinzani
mkubwa ikicheza na Simba na Yanga na kufungwa kwa tabu, tena kukiwa na dalili
za wapinzani wao kubebwa kidogo na marefa katika mechi zote, hilo linaweza kuwa
gumu.
Kitu kimoja tu, Azam imekuwa na rekodi nzuri kwenye Uwanja
wake, Chamazi na kwa sababu keshokutwa kipute kitapigwa hapo, timu hiyo ya Said
Salim Bakhresa na familia yake inaweza kupaa kileleni.
Azam ni bora, na ndiyo maana kila mashindano inayoshiriki
tangu mwaka jana imekuwa ikifika mbali.
Ina Medali za Fedha za Ligi Kuu, Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati,
Kombe la Kagame na Kombe la Urafiki na pia hawa ni mabingwa wa Kombe la
Mapinduzi.
Wawakilishi hao wa Tanzania kwenye Kombe la Shirikisho
mwakani, wanajivunia kikosi chao kizuri chenye wachezaji bora kama mfungaji bora
wa Ligi Kuu, John Bocco ‘Adebayor’, Kipre Tchetche, Salum Abubakar ‘Sure Boy
Jr.’ na wengineo.
Lakini pia kocha mtaalamu, hodari na mchapakazi, Mserbia,
Boris Bunjak ambaye Jumamosi alikuwapo Uwanja wa Taifa kuitathmini Ruvu
Shooting ilipokuwa ikicheza na Yanga na kufungwa kwa mbinde 3-2.
Hadi sasa Bunjak ameiongoza Azam FC katika mechi 14, kati ya
hizo saba za Ligi Kuu, ambazo ameshinda tano na kutoa sare mbili, zote ugenini
2-2 na Toto African mjini Mwanza na 0-0 na Prisons mjini Mbeya.
Timu moja tu ambayo imemfunga Bunjak hadi sasa, Simba SC
katika mechi tatu, moja ya michuano ya BancABC Sup8R, 2-1, Ngao ya Jamii 3-2 na
mchezo wa kirafiki 3-2 pia. Kwa ujumla kulingana na mwenendo wa Ligi Kuu hadi
sasa, Azam ikiwa imecheza mechi saba, imeonyesha msimu huu ‘haitaki masihara’.
REKODI YA
BORIS BUNJAK AZAM
Azam 2-1 Polisi (BancABC)
Azam 2-1 Simba B (BancABC)
Azam 8-0 Trans Camp (Kirafiki)
Azam 1-0 Prisons (Kirafiki)
Azam 2-0 Coastal Union (Kirafiki)
Azam 2-3 Simba SC (Ngao
ya Jamii)
Azam 1-0 Kagera Sugar (Ligi
Kuu)
Azam 2-2 Toto African (Ligi
Kuu)
Azam 3-0 JKT Ruvu (Ligi
Kuu)
Azam 1-0 Mtibwa Sugar (Ligi
Kuu)
Azam 1-0 African Lyon (Ligi Kuu)
Azam 2-3 Simba SC (Kirafiki)
Azam 1-0 Polisi (Ligi Kuu)
Azam 0-0 Prisons (Ligi Kuu)