Azam FC |
Na Mahmoud Zubeiry
AZAM FC wamepania kuifunga Simba SC kesho katika mchezo wa
Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ili kupanda
kileleni mwa ligi hiyo.
Kocha Boris Bunjak kutoka Serbia amekuwa akiwaandaa vizuri
vijana wake kwa mazoezi na kisaikolojia pia kuelekea mchezo huo, unaotarajiwa kuwa
mkali na wa kusisimua.
Azam ipo kambini kwake, Chamazi ikijifua vikali na wachezaji
wameweka kambi hapo, kwa ajili ya Ligi Kuu.
Kiboko ya nyavu za Simba na Yanga, John Raphael Bocco ‘Adebayor’
yuko fiti kupita maelezo na kiungo bora Afrika Mashariki na Kati kwa sasa,
Salum Abubakar ‘Sure Boy’ aliyekuwa majeruhi mwanzoni mwa msimu sasa amepona kabisa.
Kiungo Abdulhalim Humud aliyekuwa anasumbuliwa na maumivu
katika mechi tatu zilizopita kwa sasa yuko fiti kabisa na habari njema zaidi ni
kwamba, kiungo mwingine Mzanzibari Abdi
Kassim ‘Babbi’ amerudi kwenye fomu na anafumua mashuti makali na ya mbali ya
hatari.
Viungo washambuliaji kutoka Ivory Coast, Kipre Herman Tcheche
na Kipre Michael Balou wote wapo fiti sawa na makipa Deo Munishi ‘Dida’,
Mwadini Ally, mabeki Ibrahim Shikanda, Erasto Nyoni, Said Mourad na Aggrey
Morris.
Kwa ujumla Azam iko tayari kwa mechi hiyo ya kesho ambayo
wamepania kushinda ili kulipa kisasi cha kufungwa na Simba katika Kombe la
BancABC Sup8R.
Simba yenyewe inaendelea vizuri na kambi yake visiwiani Zanzibar
kujiandaa na mchezo huo na inatarajiwa kurejea kesho mchana na moja kwa moja
kuelekea uwanjani kukipiga.