Na Mahmoud Zubeiry
BAO la dakika ya 70 la M. Ben Mansour limezima ndoto za
chipukizi wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta na Thomas Emmanuel Ulimwengu kuwa
Watanzania wa kwanza kucheza Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, baada ya timu
yao Tout Puissant Mazembe kutupwa nje ya mashindano hayo na wenyeji Esperance
ya Tunisia kwa jumla ya bao 1-0.
Mchezo wa kwanza wiki mbili zilizopita, TP Mazembe
walilazimishwa sare ya bila kufungana mjini Lubumbashi.
Kikosi cha Simba SC kilicheza Nusu Fainali ya michuano hiyo,
wakati bado inaitwa Klabu Bingwa Afrika na kikatolewa na Mehallal El Kubra kwa
mikwaju ya penalti, baada ya sare ya jumla ya 2-2.
Lakini leo, wachezaji wawili wa Tanzania walikuwa wanajribu
kuweka rekodi mpya, ikashindikana katika mchezo ambao, marefa walionekana
dhahiri kuwabeba wenyeji.
Hata bao lenyewe la ushindi ni la utata, kwani mfungaji
alimvaa kipa Kidiaba Mutyata akiwa anaelekea kuudaka mpira na kuupiga kwa
kuinua miguu kuusindikiza nyavuni. Kidiaba aliumia baada ya hapo na kutibiwa
kwa zaidi ya dakika tano, lakini akashindwa kuendelea na mchezo na nafasi yake
ikachukuliwa na Matampi dakika ya 76.
Alitoka uwanjani huku amefungwa kamba mkono, ambao uliumizwa
katika purukushani hiyo. Pamoja na matokeo hayo, Mazembe watatakiwa kujilaumu
wenyewe kwa kutocheza kwa utulivu, muda mwingi wakibutua mipira, jambo ambalo
liliwapa kazi rahisi wapinzani wao kuwashambulia.
Haikuwa Mazembe ile ambayo wengi wanaijua inayocheza kwa
kujiamini, leo walicheza kwa kujihami zaidi- kana kwamba walikuwa wanataka sare
na kwa bahati mbaya, bao hilo lilizima ndoto zao.
Angalau baada ya kufungwa, Mazembe ilionekana kufanya mashambulizi
ya kutafuta bao, lakini tayari wapinzani wao ‘wakapaki basi’ na hivyo kushindwa
hata kuuingia ukuta wa Watunisia hao, ambao baada ya kupata bao la kuongoza
walianza kupoteza muda kwa kujiangusha uwanjani.
Samatta alikuwapo uwanjani tangu filimbi ya kwanza, lakini
Ulimwengu aliingia dakika ya 67 kuchukua nafasi ya Lusadisu.
Esperance sasa ambao ni mabingwa watetezi, wanamsubiri
mshindi wa kesho kati ya wenyeji Al Ahly ya Misri na Sunshine Stars ya Nigeria
wakutane naye katika fainali. Mchezo wa kwanza Nigeria, Ahly walilazimisha sare
ya kufungana mabao 3-3, hivyo wanapewa nafasi kubwa ya kukutana na Waarabu
wenzao wa Afrika katika mechi ya mwisho.