Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga akizungumza na Waandishi asubuhi hii. kulia ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji, Tito Osoro |
MABOSI WAPYA; Kulia ni Oundo na kushoto Mwalusako |
Na Mahmoud Zubeiry
KLABU ya
Yanga imetangaza rasmi kumfukuza Kocha wake Mkuu, Mbelgiji Tom Saintfiet na nafasi
yake atakaimu Msaidizi wake, Freddy Felix Minziro hadi hapo atakapopatikana
kocha mwingine.
Makamu Mwenyekiti
wa Yanga, Clement Sanga amesema asubuhi hii katika Mkutano na Waandishi wa
Habari makao makuu ya klabu, makutano ya mitaa ya Twiga na Jangwani kwamba,
matokeo mabaya ndio yamefanya Saintfiet asitishiwe mkataba.
Aidha, Sanga
alikanusha madai kwamba eti kocha huyo amefukuzwa baada ya kutofautiana na
Mwenyekiti wa klabu, Yussuf Manji.
“Timu
ilipokwenda Mbeya, ikatoka sare na Prisons akalalamikia huduma, lakini sisi
taarifa tulizozipata, yeye aliwaruhusu wachezaji kwenda kulewa baada ya mechi. Kuna mapungufu
mengine mengi, ambayo hatuwezi kusema hadharani.
Kwa mfano
timu ilipotoka Mbeya, tulitaka iende moja kwa moja Morogoro, yeye akalazimisha
timu irudi Dar es Salaam, tena iende tena Morogoro. Wachezaji wakachoka sana na
hii tunaamini ilichangia hata kufungwa na Mtibwa.
Timu iliporudi
kutoka Morogoro, tukaamua iingie kambini, yeye akapinga akisema timu kubwa kama
Barcelona Ulaya, hazikai kambini, yaani anataka atupangie kazi sisi, tukaona
huyu mtu haendani na maadili ya uongozi na hatufai, tukaamua kusitisha mkataba
wake,” alisemsa Sanga.
Saintfiet
ameiongoza Yanga katika mechi 14 tu ndani ya siku 80 tangu ajiunge nayo Julai
mwaka huu, akirithi mikoba ya Mserbia, Kostadin Bozidar Papic na katika mechi
hizo amefungwa mbili tu, dhidi ya Mtibwa 3-0 na Atletico ya Burundi 2-0.
Katika mechi
hizo, zimo sita za Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame,
ambazo aliiwezesha Yanga kutwaa taji, ikipoteza mechi moja tu dhidi ya Atletico
ya Burundi.
Pamoja na
kufukuzwa kwa kocha, Yanga imemtangaza rasmi beki wa zamani wa Yanga na timu ya
taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Lawrence Mwalusako kukaimu nafasi ya Katibu wa
klabu hiyo na Dennis Oundo kuwa kaimu Mkurugenzi wa Fedha na Utawala.
Hatua hiyo,
inafuatia kusimamishwa kazi kwa Sekretarieti nzima ya klabu, akiwemo Katibu Celestine
Mwesigwa na Ofisa Habari, Louis Sendeu, kutokana na kile ilichoeleza utendaji
usioridhisha.
Wengine waliokumbwa
na panga hilo ni Masoud Saad, aliyekuwa Ofisa Utawala, Philip Chifuka aliyekuwa
Mhasibu na Hafidh Saleh aliyekuwa Meneja ambaye anahamishiwa kwenye majukumu
mengine.
Mbali na Mwalusako
na Oundo, kiungo wa zamani wa klabu hiyo, Sekilojo Johnson Chambua anatajwa
kupewa nafasi ya Umeneja, wakati nafasi ya Msemaji wa klabu iliyoachwa wazi na
Louis Sendeu, inaelezwa atapewa mdogo wa mke wa Ridhiwani Kikwete, aliyehesabu
kura za Abdallah Bin Kleb katika uchaguzi mdogo wa klabu, Julai 14.
0 comments:
Post a Comment