Baadhi ya wachezaji wa Yanga |
Na Mahmoud Zubeiry
YANGA ya Dar es Salaam, inatarajiwa kuingia kambini wilayani Bagamoyo mkoani Pwani leo, kujiandaa na mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya wapinzani wao wa jadi, Simba SC , Oktoba 3, mwaka huu.
Habari kutoka ndani ya Yanga, zimesema kwamba timu hiyo itaingia kwenye mchezo wa kesho dhidi ya African Lyon, ikitokea Bagamoyo na baada ya mechi itarejea huko kuendelea kujiandaa na pambano la watani.
Mechi hiyo inatarajiwa kuwa kali na ya kusisimua, kwa sababu mara ya mwisho timu hizo zilipokutana, Yanga ilifungwa mabao 5-0 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kipigo hicho ilidaiwa kilitokana na uongozi dhaifu chini ya Mwenyekiti, Wakili Lloyd Baharagu Nchunga na pia ilikuwa sababu ya kumuondoa madarakani kiongozi huyo na kufanyika uchaguzi mdogo, uliomuweka madarakani Yussuf Manji, Mwenyekiti mpya.
Tangu wakati wa kampeni, miongoni mwa mambo ambayo wana Yanga wamekuwa wakiomba kutoka kwa Manji ni kulipiwa kisasi cha 5-0, ingawa kwa hali ya sasa ya timu hizo, ubora wao haupishani sana, hakuna hakika kama hilo litawezekana.
0 comments:
Post a Comment